Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Patience Ntwina akizungumza leo Aprili 09, 2025 wakati akifungua mafunzo muhimu kwa watumishi wa Tume kuhusu usimamizi na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari kwa wavuvi wadogo wadogo sambamba na kuzingatia haki za binadamu. Mafunzo haya yanafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Four Points jijini Dar es Salaam.
.jpeg)
Matukio mbalimbali wakati wa magunzo ya kutengeneza uelewa juu ya haki za binadamu za wavuvi wadogo wadogo.

Picha ya pamoja.
KATIBU Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Patience Ntwina amesema kuwa Jukumua la kulinda na kuhifadhi haki za binadamu na rasilimali za bahari si la Serikali au THBUB pekee, bali linahitaji ushirikiano wa wadau wote katika jamii.
Hayo ameyasema jijini Dar es Salaam leo Aprili 09, 2025 wakati akifungua mafunzo muhimu kwa watumishi wa Tume kuhusu usimamizi na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari kwa wavuvi wadogo wadogo sambamba na kuzingatia haki za binadamu. Mafunzo haya yanafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Four Points.
Ntwina ameeleza kuwa mafunzo hayo ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya THBUB na Taasisi ya Haki za Binadamu ya Denmark (Human Rights Institute of Denmark) ‘DIHR’ kupitia mradi wa Haki za Binadamu na Biashara (Business and Human Rights), unaolenga kujenga uelewa juu ya usimamizi shirikishi na unaozingatia haki katika matumizi ya rasilimali za bahari. Mradi huu unatekelezwa kwa kipindi cha 2024 hadi 2027 kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Uswisi (Sida).
“Mradi huu unalenga jamii za wavuvi wadogo wadogo kwa kuzingatia mazingira yao ya kazi na changamoto wanazokumbana nazo, na Tanzania kupitia THBUB ni miongoni mwa nchi zinazotekeleza mradi huu baada ya Senegal na Ghana” Amesema Ntwina.
Pia amebainisha kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea watumishi uwezo wa kushughulikia masuala ya haki za binadamu katika usimamizi wa rasilimali za bahari, ikiwemo kufanya tathmini ya hali ya wavuvi, kuchambua sera na sheria zinazohusiana na sekta ya uvuvi na kutoa mapendekezo ya maboresho.
Ntwina Mafunzo haya pia yanatarajiwa kusaidia katika kuzuia na kutatua migogoro kati ya wavuvi wadogo na mamlaka mbalimbali, kwa kuhakikisha kuwa haki zao zinazingatiwa katika mipango ya matumizi bora ya rasilimali za bahari.
Pia ametoa wito kwa washiriki kushiriki kikamilifu ili kutoa mchango wenye tija kwa maendeleo endelevu ya sekta ya uvuvi na kulinda haki za binadamu kwa wote.
Kwa upande wa mshiriki Juma Mrelu kutoka Mtwara amesema kuwa mafunzo hayo yatamwezesha kupata uelewa ili akaweze kuwaelimisha wavuvi wadogo wadogo pamoja na wafanyabiashara wa mazao ya samaki ili waweze kujua haki zao katika ufanyaji shughuli mbalimbali katika fukwe za bahari.