Na Benny Mwaipaja, Warsaw-Poland
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameishukuru Serikali ya Poland kupitia Shirika lake la Bima (KUKE), kwa kuonesha nia ya kudhamini upatikanaji wa fedha kwa ajili ya Ujenzi wa kipande cha 3 na cha 4 cha Mradi wa Reli ya Kisasa wa SGR kuanzia Makutupora hadi Tabora na kinachoanzia Tabora hadi Isaka.
Dkt. Nchemba alitoa shukrani hizo Mjini Warsaw nchini Poland, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Poland (KUKE), Bw. Janusz Wladyczak, alipokuwa akihitimisha ziara yake ya kikazi katika nchi za Italy, Ufaransa na Poland, iliyolenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na nchi hizo.
Alisema kuwa upatikanaji wa fedha hizo utawezesha ukamilishaji kipande cha 3 (lot 3) cha reli chenye urefu wa km 294, kutoka Makututupora ya mkoani Singida hadi Tabora na kipande kingine cha 4 (lot 4) chenye urefu wa kilometa 130, kutoka Tabora hadi Isaka.
“Mradi huu wa kimkakati ni daraja litakalo ifungua nchi yetu kibiashara na nchi tunazopakana nazo zinazotumia Bandari ya Dar es salaam, kwa kuziba pengo la uhaba wa usafiri wa njia ya reli kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na kukuza soko la bidhaa katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Maziwa Makuu, ikiwemo Uganda, Burundi na DRC Congo” alisema Dkt. Nchemba.
Alifafanua kuwa Ujenzi wa kipande cha 1 na cha 2 cha SGR (Dare Salaam-Morogoro-Dodoma – Makutupora) uliogharimu dola za Marekani bilioni 3.14 umekamilika na huduma za reli zimeanza kutolewa tangu Julai mwaka jana (2024), huku kipande cha 3 hadi 7 cha Reli hiyo kuelekea mkoani Mwanza kitakachogharibu dola za Marekani bilioni 8.6 uko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali inatafuta fedha kutoka vyanzo mbalimbali ili kuwezesha kukamilisha mradi huo mkubwa wa kimkakati na kuishukuru Poland, Kupitia Shirika lake la Bima (KUKE) kwa kuitafutia Serikali fedha za kukamilisha mradi huo utakaochangia kukuza biashara, ajira na hatimaye uchumi wa wananchi na nchi husika zinazoguswa na miundombinu ya Reli hiyo.
Aidha, katika kikao chao, aliliomba Shirika hilo kuwashawishi wawekezaji kutoka Poland kushirikiana na Serikali pamoja na Sekta Binafsi ya Tanzania kuwekeza katika miradi mingine yenye tija hususan katika sekta za kilimo, nishati, maji, afya, utalii na ujenzi wa miundombinu mingine ya viwanda vya uzalishaji bidhaa kwa faida ya nchi hizo mbili kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Poland (KUKE), Bw. Janusz Wladyczak, alibainisha kuwa Poland iko tayari kushiriki katika Ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR kutokana na umuhimu wake kiuchumi kwa Tanzania na nchi Jirani na kuahidi kuwa Poland iko tayari pia kushirikiana na Tanzania kwenye miradi mingine ya maendeleo kupitia Serikali kwa Serikali na wawekezaji binafsi.
Alisema kuwa nchi yake imebobea katika kilimo, uzalishaji wa bidhaa za mifugo, teknolojia ya nishati, madini na bidhaa nyingine kadha wa kadha zinazozalishwa kwa gharama nafuu na ubora wa hali ya juu na kwamba wawekezaji kutoka nchini humo wako tayari kuwekeza Tanzania.
Naye alitoa rai kwa kampuni za Kitanzania, kuwekeza nchini Poland ambapo utaratibu wao ni kwamba kampuni itakayowekeza nchini humo itapewa hadhi ya kuwa Kampuni ya Kipoland na kupewa fursa ya kufaidi soko kubwa la bidhaa la nchi za Jumuiya ya Ulaya.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Poland (KUKE), Bw. Janusz Wladyczak, Makao Makuu ya Shirika hilo Jijini Warsaw, Poland, ambapo ameishukuru Serikali ya Poland kupitia Shirika hilo kwa kuonesha nia ya kudhamini upatikanaji wa fedha kwa ajili ya Ujenzi wa kipande cha 3 na cha 4 cha Mradi wa Reli ya Kisasa wa SGR kuanzia Makutupora hadi Tabora na kinachoanzia Tabora hadi Isaka.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha, Warsaw-Poland)