Watumishi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wamepongezwa kwa kuwa moja ya taasisi za umma zinazoendesha Baraza la Wafanyakazi lenye tija, ambalo limeendelea kuwa kichocheo cha maamuzi makubwa ya kuboresha huduma za usafiri wa anga nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Msajili wa Hazina, Bw. Nehemia Mchechu, wakati wa ufunguzi wa Baraza la Pili la Wafanyakazi la TCAA kwa mwaka wa fedha 2024/2025, lililofanyika Aprili 10, 2025, jijini Dodoma.
Bw. Mchechu alisisitiza umuhimu wa vikao vya Baraza katika kuimarisha misingi ya demokrasia sehemu za kazi na kuwahamasisha wajumbe kuhakikisha wanawasilisha mrejesho kwa watumishi wenzao waliowawakilisha ili kujenga mshikamano na ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.
“Baraza hili si tu jukwaa la mijadala, bali ni daraja la kuelekea maboresho ya kweli ya mazingira ya kazi. Mnapaswa kulitumia kama chombo cha kuleta mabadiliko chanya, lakini pia kuhakikisha kila mtumishi anapata fursa ya kushiriki katika safari ya maendeleo ya taasisi,” alisema Bw. Mchechu.
Aidha, aliipongeza menejimenti ya TCAA kwa kujenga mazingira mazuri ya kazi na kuwezesha ufanisi wa Baraza hilo, akisema kuwa hatua hiyo ni mfano wa kuigwa na taasisi nyingine.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Bw. Salim Msangi, akimkaribisha Bw.Mchechu alieleza kuwa Mamlaka itaendelea kuboresha mazingira ya kazi ili kila mtumishi aweze kutimiza wajibu wake kwa weledi na kuisukuma mbele sekta ya usafiri wa anga.
“Menejimenti inatambua mchango wa kila mmoja wenu. Ni muhimu kila mtumishi afahamu kuwa TCAA inajengwa kwa juhudi za pamoja. Naomba tushirikiane, tusaidiane inapobidi, kwa kuwa tunalenga kuhakikisha malengo ya taasisi na Serikali kwa ujumla yanafikiwa na huduma bora inatolewa kwa Watanzania,” alisema Bw. Msangi.
Baraza la wafanyakazi lina lengo la kuendeleza mawasiliano ya wazi kati ya menejimenti na watumishi, pamoja na kujadili mikakati ya kuboresha huduma, mazingira ya kazi, na ufanisi wa taasisi.
Katika kuimarisha uelewa wa maendeleo ya sekta ya anga, wajumbe wa Baraza pia watapata fursa ya kufanya ziara ya kutembelea na kujionea hatua ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, uliopo jijini Dodoma. Ziara hiyo inalenga kuwapa watumishi uelewa wa kina kuhusu juhudi za serikali na mchango wa TCAA katika kukuza miundombinu ya usafiri wa anga nchini.
Msajili wa Hazina, Bw. Nehemia Mchechu akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la TCAA wakati wa kufungua kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Takwimu House Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Bw. Salim Msangi akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la TCAA wakati wa ufunguzi wa kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Takwimu House Dodoma.
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la TCAA wakiwa katika picha za pamoja na meza kuu
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la TCAA kwa pamoja wakiimba nyimbo ya mshikamano