Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Ukraine zimekubaliana kuongeza ushirikiano katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii ikiwemo kilimo, biashara na uwekezaji, viwanda, utalii, elimu na afya kwa maslahi ya pande zote mbili.
Makubaliano hayo yamefikiwa kwenye mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Mhe. Andrii Sybiha yaliyofanyika nchini Uturuki pembezoni mwa Mkutano wa 4 wa Diplomasia wa Antalya (The Antalya Diplomacy Forum – ADF2025).
Katika mazungumzo hayo Waziri Kombo amebainisha kuwa ni wakati muafaka kwa pande zote mbili kuimarisha mazingira yatakayonufaisha wananchi kiuchumi.
“Tanzania inafahamika na kusifika kote duniani kuwa ni rafiki wa wote, hivyo tutaendelea kudumisha na kufungua zaidi milango ya ushirikiano kwa Ukraine na washirika wengine wa maendeleo ili kuboresha maisha ya watanzania. Tuataendelea kuwavutia zaidi wawekezaji na watalii, kutafuta fursa za mafunzo na masomo nje ya nchi na soko la bidhaa zinazozalishwa na wananchi wetu ili kukuza uchumi wao na pato la taifa”. Alieleza Waziri Kombo.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine ameeleza kuwa Tanzania ni mshirika muhimu kwa Ukraine kutokana msimamo wake thabiti na umahiri wake katika kusimamia agenda za msingi katika majukwaa ya kimataifa ikiwemo masuala ya amani na usalama.
Aliongeza kuwa Ukraine ipo tayari kuongeza maeneo ya ushirikiano wa kiuchumi na Tanzania ikiwemo sekta ya ujenzi wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji kwa manufaa ya pande zote mbili.
Waziri Kombo yupo ziarani nchini Uturuki ambapo pamoja na masuala mengine anashiriki katika Mkutano wa 4 wa Diplomasia wa Antalya (The Antalya Diplomacy Forum – ADF2025) unaoendelea nchini humo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Mahmoud Thabit Kombo akijadili jambo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Mhe.Andrii Sybiha walipokutana kwa mazungumzo pembezoni mwa Mkutano wa ADF2025 jijini Antalya, Uturuki.
Mazungumzo yakiendelea
.jpg)