Mabalozi wanaowakilisha nchi mbalimbali pamoja na mashirika ya kimataifa wameonesha kuvutiwa na vivutio vilivyoko nchini, huku wakiahidi kuiongezea nguvu Tanzania katika kutangaza vivutio hivyo kwenye nchi wanakotoka.
Wakizungumza jana katika hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Benki ya NMB kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, mabalozi hao wamesema Tanzania imebarikiwa kwa kiasi kikubwa katika utunzaji wa bioanuai – hali inayochangia ustawi wa mazingira na wanyama pori.
Hafla hiyo ilikuwa sehemu ya ziara ya siku tatu ya kutembelea vivutio mbalimbali nchini, iliyopewa jina la Diplomatic Safari Tour, na imefanyika jijini Arusha.
Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Issack Njega, ameishukuru Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuandaa ziara hiyo, akieleza kuwa itakuwa na mafanikio makubwa katika kuitangaza Tanzania kama kivutio cha kipekee cha utalii.
“Tumeona vivutio vingi katika Hifadhi ya Serengeti – hifadhi kubwa zaidi Afrika, yenye hadhi na sifa kubwa duniani hadi kupata tuzo nyingi. Na sisi tumekubali kuwa inastahili kwa upekee wake,” amesema.
Ameongeza kwa kuiomba Serikali ya Tanzania kuimarisha mashirikiano na Kenya katika kutangaza vivutio vya pamoja, hasa vile vinavyovuka mipaka kama Serengeti, ambayo inapakana na Hifadhi ya Masai Mara ya Kenya – maeneo yanayoshuhudia misafara mikubwa ya nyumbu.
Balozi wa Burundi nchini Tanzania, Mhe. Leontine Nzeyimana, amesema mafanikio ya Tanzania katika utunzaji wa bioanuai yamekuwa rafiki kwa wanyama na kuleta uasili wake wa kipekee. Ameahidi kuhamasisha wananchi wa Burundi kutembelea vivutio vya Tanzania.
“Mimi binafsi sijawahi kufika Serengeti wala Ngorongoro. Nilikuwa naogopa kupanda puto (balloon), lakini nilipohamasishwa na kujaribu, nimefurahia sana. Nitarejea tena na tena – na kuwaleta wenzangu wengi.”
Amesema raia wengi wa Burundi hutumia gharama kubwa kwenda Ulaya kwa ajili ya mapumziko, ilhali Tanzania ina upekee huo huo – au zaidi.
“Pale Ngorongoro nimeona Watanzania walivyobarikiwa, hasa baada ya kubahatika kuwaona wanyama wakubwa watano (Big Five) kwa wakati mmoja. Nitakapofika Burundi nitawaambia wenzangu kuwa hapa ndipo mahali sahihi – na si ghali, kwani watatozwa bei ya mwanajumuiya wa Afrika Mashariki.”
Balozi wa Comoro, Dkt. Ahamada El Badaoui Mohamed, amesema amefurahia sana kutembelea Serengeti na Ngorongoro na kuvutiwa na wanyama pamoja na mazingira asilia, ambayo amesema yanaweza hata kuwa tiba ya msongo wa mawazo.
“Nimetembelea nchi nyingi zenye wanyama, lakini Tanzania ina upekee wa asili – kuanzia bioanuai ya wanyama, wadudu hadi mimea. Nimevutiwa zaidi na mazingira ya asili,” amesema na kuongeza:
“Naishauri Tanzania kuongeza nguvu katika kutangaza vivutio hivi. Mkifanikiwa, mnaweza kuwa nchi iliyoendelea kwa kutegemea utalii pekee. Uzuri ni kwamba mimi naenda kuanza kuwatangaza – na naahidi wengi watakuja.”
Naye Mkuu wa Kitengo cha Miamala ya Kibenki kutoka NMB, Bi. Linda Teggisa, amesema lengo la kuwakutanisha mabalozi na wakuu wa misheni za kidiplomasia pamoja na wawakilishi wa taasisi za kimataifa ni kuwaeleza kuhusu masuluhisho ya kifedha – hususan ya kidijitali – ambayo NMB inatoa kwa sekta ya utalii.
“Tumewaeleza kuhusu masuluhisho yenye mlengo wa kujenga uwezo wa kifedha kwa wawekezaji – kama mikopo ya kununua magari na vifaa vingine muhimu kwa shughuli za utalii.”
Ameongeza kuwa kwa sasa, NMB inawekeza zaidi katika huduma za kidigitali ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia.
“Zaidi ya asilimia 94 ya miamala yetu sasa inafanyika kidigitali. Tunawekeza nguvu zaidi huko kuhakikisha hakuna mteja anakwama kupata huduma – popote alipo ndani au nje ya nchi,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, amesema wizara imeandaa ziara hiyo kwa lengo la kuwapa fursa wadau wa kidiplomasia kuona vivutio vya Tanzania kama njia ya kukuza mahusiano na utalii.
“Utalii unazidi kuwa uti wa mgongo wa uchumi wetu. Kwa sasa unachangia asilimia 25 ya pato la taifa, na tunalenga kuongeza hadi kufikia nusu ya mapato yote, kwa kufikia zaidi ya watalii milioni saba kwa mwaka.”
Ameeleza kuwa katika awamu ya kwanza ya ziara hiyo, wameshiriki wajumbe 25 kutoka nchi mbalimbali, na lengo ni kuwashirikisha wajumbe wote 93 walioko na wanaoshirikiana na Tanzania.
“Wamepata nafasi ya kutembelea Serengeti, Ngorongoro, na sasa wanakwenda Zanzibar kushuhudia vivutio vilivyopo huko pia. Tunaamini watakuwa mabalozi wazuri wa nchi yetu,” amesema Balozi Mussa.