Na Mwandishi Wetu; Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amesema katika mwaka wa fedha 2025/26, Serikali itaanza kutumia Mfumo wa kieletroniki ambao utawezesha watanzania kupata taarifa kuhusu fursa za ajira zilizopo nje ya nchi.
Amesema, mfumo huo pia utaisaidia Serikali kupata taarifa za Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na kujua nchi wanakofanya kazi, aina ya kazi wanazozifanya, na taarifa zao nyingine muhimu zitakazounganishwa na mifumo ya kibenki ili kurahisisha ufuatiliaji wa marejesho ya fedha (remittances) zinazotumwa nchini.
Mhe. Kikwete ametoa kauli hiyo Aprili 15, 2025, bungeni wakati akichangia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Amesema kuwa, mfumo huo utaiwezesha Serikali kufahamu kwa usahihi kiwango cha fedha kinacholetwa nchini na Watanzania wanaoishi ughaibuni, pamoja na kusaidia kutambua fursa zaidi za ajira ambazo Watanzania wanapaswa kuzichangamkia.
Ameongeza kuwa mfumo huo utaunganishwa na mifumo mingine ya Serikali kama vile Mfumo wa Usajili wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA), vyeti vya kuzaliwa, uhamiaji, na mamlaka za elimu, ili kurahisisha taratibu za kuomba ajira nje ya nchi.
“Moja ya jambo kubwa ambalo Bunge lako tukufu limekuwa likilizungumzia kwa sauti ya juu ni kiasi kidogo cha fedha kinachorejeshwa nchini kutoka kwa Watanzania wanaofanya kazi nje ya nchi. Niwahakikishie kuwa moja ya sababu kuu ni kukosekana kwa mfumo thabiti wa kupata taarifa za watu hao, ni wangapi, wanafanya nini na wapi, pamoja na fedha kiasi gani wanazorejesha,” amesema Mhe. Kikwete.