Katibu Mtendaji Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Fred Msemwa,akiwa katika mazungumzo na Spika wa Bunge na Rais wa umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson leo Aprili 16,2025 Jijini Dodoma mara baada ya kwenda Ofisini kwa Mhe.Spika bungeni Dodoma.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Katibu Mtendaji Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Fred Msemwa amekutana na Spika wa Bunge na Rais wa umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson ambapo amesema katika mazungumzo yao wamegusia mambo watakayoyapa kipaumbele kila siku za ufanyaji kazi wa tume hiyo.
Dkt. Msemwa ameyabainisha hayo leo Aprili 16,2025 Jijini Dodoma mara baada ya kukutana na kujitambulisha kwa Spika huyo ambapo aliteuliwa Februari 27,2025 na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuchukua nafasi ya Lawrence Mafuru aliyefariki Novemba 9 mwaka jana.
“Namshukuru sana Mhe. Spika kwa ushirikiano mkubwa ambao amekuwa akiutoa kwa Tume ya Taifa ya Mipango kupitia kamati zake na tumepata michango muhimu sana iliyoboresha mpango wetu wa maendeleo wa mwaka 2025/26 na kupitia michango hiyo ya wabunge tutarajie bajeti yetu kuwa na mrejesho huo muhimu kutoka kwa wawakilishi hao wa wananchi ili nchi yetu izidi kupiga hatua na wadau muhimu wa maendeleo katika taifa letu,”amesema.
Aidha, amesema kuwa kwa upande wa majadiliano ya bajeti yanayoendelea watarajie matokeo mazuri hasa yanayotokana na Wabunge katika bajeti ambayo imekuwa ikiwasilishwa na Serikali na kuongeza kuwa katika mpango wa maendeleo wa mwaka 2025/26 uliowasilishwa Bungeni na Prof. Kitila Mkumbo kamati ya Bunge ya bajeti ilitoa mchango mzuri ambao umeleta maboresho katika namna ambayo inakidhi matarajio ya wadau muhimu.
“Kwahiyo kinachofanyika hapa ni kuhakikisha kwamba wawakilishi wa wananchi wanatoa mawazo ya nini hasa kifanyike katika mwaka ujao wa fedha ili kupitia michango hiyo maana yake hizo ni sauti za wananchi, kwahiyo sauti za wananchi zikiingia katika mipango yetu tunakuwa tunafanya yale yanayotarajiwa na wananchi,”ameongeza.
Pia Dkt. Masemwa amebainisha kuwa anatarajia bajeti zitakazoidhinishwa na Bunge katika mwaka ujao wa fedha kuwa na sauti za wananchi na kupitia sauti hizo bajeti itakuwa inaakisi maendeleo ya nchi hivyo hapana shaka watafikia malengo wanayotarajia na yatawagusa wananchi.
Kwa upande wake Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson amesema kuwa Serikali ina matarajio makubwa kwa Tume ya Taifa ya Mipango katika kusimamia mipango na masuala ya maendeleo ya kiuchumi, kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi na jiografia ya nchi, ili kuhakikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na malengo yaliyoainishwa katika Mpango Elekezi wa Maendeleo wa 2050.