NA WILLIUM PAUL, SAME.
WANANCHI wamesisitizwa kujijengea utamaduni wa kuwakumbuka na kuwajali watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwa kuwapatia msaada wa mahitaji ya msingi hususan chakula na mavazi ili nao wajisikie kuwa sehemu ya jamii na wenye thamani.
Wito huo umetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, KasildaMgeni wakati alipotembelea na kutoa sadaka yake ya chakula na vinywaji kuelekea sikukuu ya Pasaka katika kituo cha Rafiki cha kulelea watoto Yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi (Rafiki Children Centre) kilichopo wilayani humo.
“Hawa watoto hawakupenda kuwa katika mazingira haya, ila walijikuta wapo katika mazingira haya, Niwaombe sana wanasame, pamoja na raha zenu zote, mkumbuke kuwa watoto pia wamahitaji raha kama.unazozipata, basi zile raha unazozipata wape na watoto wa kituo hiki (Watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi)”. Alisema Kasilda.
Pia Kasilda amewashukuru na kuwapongeza walezi na wasimamizi wa kituo hicho kwa kuonesha moyo wa upendo ambapo amewaahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana nao katika hali zote ili kufanikisha ndoto za watoto wanaolelewa kituoni hapo.
Naye Jeremia letus, ambaye ni Afisa ustawi wa jamii na Msimamizi wa kituo cha Rafiki amemshukuru mkuu wa Wilaya ya Same kwa kuendelea kuwa sehemu ya faraja katika kituo hicho katika utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Pamoja na mambo mengine ameeleza kuwa wameweka kipaumbele kwa watoto wanaolelewa kituoni hapo kuhakikisha wanapata elimu huku akiongezea kuwa wanakabiliwa na changamoto ya jengo kwa ajili ya watoto hao.
Kituo cha Rafiki cha kulelea watoto Yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi kina jumla ya watoto ishirini mpaka sasa.