
Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini zimekatiza tena mawasiliano ya barabara kuu ya Dar es Salaam – Lindi, katika eneo la Somanga, kuanzia mchana hadi jioni ya leo, Aprili 16, 2025. Kwa sasa hakuna gari linaloweza kupita, hali iliyosababisha msongamano mkubwa wa magari na usumbufu kwa wasafiri.
Mashuhuda waliopo eneo hilo wameieleza kuwa hali ilikuwa tulivu wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipowasili eneo hilo pamoja na Waziri wa Ulinzi Dkt. Stegomena Tax na Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega. Hata hivyo, dakika chache baada ya viongozi hao kuondoka, mvua kubwa ilinyesha na kuharibu kabisa njia.
Kwa sasa, Serikali imeweka boti ndogo inayovusha watu kutoka upande mmoja hadi mwingine, lakini magari yote yamekwama – yakisubiri mvua kupungua na maji kupungua.
Ikumbukwe kuwa ujenzi wa Daraja la Somanga-Mtama unaendelea, ukiwa ni sehemu ya mkakati wa serikali kupitia TANROADS kuboresha miundombinu ya kusini mwa Tanzania. Mradi huu mkubwa unalenga kuunganisha mikoa ya Lindi, Mtwara na maeneo ya jirani, kwa njia ya kisasa – ikiwa na njia za magari, waenda kwa miguu, na taa za barabarani kwa usalama zaidi.
Kwa sasa, wananchi wanaendelea kuomba hatua za haraka ili kurejesha mawasiliano muhimu katika ukanda huo