Na. Peter Haule, WF, Dodoma
Serikali imesema kuwa Kampuni ambazo hazijaorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) hukutana na changamoto za kutofahamu thamani halisi ya uwekezaji kutokana na kukosekana kwa ukwasi wa hisa zao.
Hayo yalisemwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Geita Mjini, Mhe. Constantine John Kanyasu, aliyetaka kujua hasara na faida kwa kampuni kutotekeleza Sheria ya kujiorodhesha kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam.
Mhe. Chande alisema kuwa Kampuni ambazo hazijajiorodhesha katika Soko la Hisa hutawaliwa na kukosekana kwa uwazi na hivyo Serikali na wanahisa kushindwa kupata taarifa stahiki za mwenendo wa biashara na fedha.
“Kwa mujibu wa Sheria, ni Kampuni ya simu pekee ndio hulazimika kuuza hisa kwa umma na kuorodheshwa katika soko la hisa isipokuwa Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa kwa asilimia 25 au zaidi na Kampuni ambazo zinatoa huduma ya minara ya simu”, alisema Mhe. Chande.
Aidha alizitaja faida za Kampuni kujiorodhesha kwenye Soko la Hisa kuwa ni pamoja na kuongeza mtaji, kuongeza ufanisi na tija, kuiwezesha Serikali kupata mapato stahiki na kutambua thamani halisi ya hisa zake ambapo wanahisa wanapata thamani ya hisa zao wanapotaka kuuza kwa kufuata mwenendo wa soko (demand and supply).
Alisema faida nyingine ni pamoja na kuwapa wananchi fursa ya kununua hisa na hivyo kuwezeshwa kushiriki katika uchumi wa nchi na kutoa fursa kwa wawekezaji wanaotaka kuuza uwekezaji wao wakati wanapohitaji fedha.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)