Na Mwandishi wetu, Magu
MWENYEKITI wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele leo Aprili 23,2025 ameongoza kikao cha pamoja kati ya Tume na Wadau wa Uchaguzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mkoani Mwanza kwa lengo la kujiridhisha iwapo taarifa zilizopo kwenye maombi yaliyowasilishwa ya kuligawa jimbo la Magu ni sahihi kuhusu jimbo husika.
”Tulipokea maombi ya mapendekezo ya kugawa jimbo la uchaguzi la Magu kupitia barua yenye Kumb. Na. CFA.89/231/01C/20 ya tarehe 11 Machi, 2025 kutoka kwa Katibu tawala Mkoa wa Mwanza, hivyo kikao hiki ni kifupi, lengo lake ni kujiridhisha na takwimu na jina la jimbo kama mlivyowasilisha ikiwa ni sehemu ya jukumu la Tume la kuwashirikisha wadau wake wa uchaguzi,”alisema Jaji Mwambegele.
Alisema, Tume imechagua kutembelea baadhi ya majimbo yaliyoomba kugawanywa kwa lengo la kujiridhisha iwapo taarifa zilizopo kwenye maombi yaliyowasilishwa ni sahihi kuhusu jimbo husika.
Jaji Mwambegele alisema kwa mujibu wa ibara ya 75(4) na 74(6)(c) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 ikisomwa pamoja na kifungu cha 10(1)(d) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 1 ya mwaka 2024, Tume ina jukumu la kuchunguza na kuigawa Jamhuri ya Muungano katika majimbo ya uchaguzi. Aidha, Tume inaweza kutekeleza jukumu hilo mara kwa mara au angalau kila baada ya miaka kumi.
”Aida, ibara ya 75(3) na (4) imeainisha vigezo vya ugawaji wa majimbo ambavyo ni idadi ya watu, upatikanaji wa mawasiliano, na hali ya kijiografia. Vigezo vingine vinavyozingatiwa na Tume katika kugawa majimbo vimeainishwa katika Jedwali la Tatu la Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za Mwaka 2024,”alisema Jaji Mwambegele.
Jaji Mwambegele alivitaja vigezo vingine vinavyohusika katika ugawaji wa majimbo kuwa ni pamoja na hali ya kiuchumi, ukubwa wa eneo la jimbo husika, mipaka ya kiutawala, jimbo moja kutokuwa ndani ya Wilaya au Halmashauri mbili, mpangilio wa maeneo ya makazi ya watu yaliyopo, mazingira ya muungano, uwezo wa ukumbi wa Bunge; na idadi ya viti maalum vya wanawake.
Miongoni mwa waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na viongozi wa Mkoa wa Mwanza, Viongozi wa Wilaya ya Magu, Viongozi wa Vyama vya Siasa Magu, Wawakilishi wa makundi mbalimbali ya wanawake, vijana, wenye ulemavu na wazee wa Kimila.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ilitangaza kuanza kwa mchakato wa kuchunguza na kugawa au kubadili majina ya majimbo ya uchaguzi ambapo ilipokea mapendekezo kuanzia tarehe 27 Februari, 2025 hadi tarehe 26 Machi, 2025.