Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, ukiongozwa na Mwenyekiti wake, Ndg. Wise Mgina, umefanya kikao muhimu cha kusainishana mikataba na wawekezaji kwa ajili ya kuanzisha mradi wa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba katika Kata ya Iwela, Kijiji cha Iwela, eneo la Chuva, pamoja na eneo la Uhonjo katika Kata ya Lupingu, kikao ambacho kimefanyika katika ofisi ya mwenyekiti wa halmashauri hiyo.
Mradi huu unalenga kutumia eneo lenye ukubwa wa mita za ujazo 21.4 katika Ziwa Nyasa kwa ajili ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba, ikiwa ni sehemu ya juhudi za halmashauri katika kukuza uchumi wa wilaya na kupambana na udumavu kwa kuongeza upatikanaji wa protini kupitia samaki.
Kikao hicho ambacho pia kilihudhuriwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Ndg. Sunday Deogratias pamoja na viongozi mbalimbali wa halmashauri hiyo ambapo usainishwaji wa mikataba hiyo ulikuwa chini ya usimamizi wa Mwanasheria wa Halmashauri, Ndg. Mathan Chalamila ili kuhakikisha kuwa mikataba hiyo inazingatia sheria na kanuni zote husika.
Akizungumza kabla ya kusainishana mikataba hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri, Ndg. Mgina, aliwashukuru wawekezaji, hususan wale wazawa wa Ludewa, kwa kuona umuhimu wa kuwekeza nyumbani. Alisisitiza kuwa uwekezaji huu utasaidia kuongeza uchumi wa wilaya na kupambana na udumavu kwa kuongeza upatikanaji wa samaki bora kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Ndg. Sunday Deogratias, alieleza kuwa mradi huu utakuwa chachu kwa wananchi wengine kuona umuhimu wa kuwekeza nyumbani. Aliongeza kuwa mradi huu utasaidia kuitangaza halmashauri sehemu mbalimbali nchini hivyo itasaidia kuongeza uchumi wa wilaya, mkoa na hata taifa kwa ujumla.
Wawekezaji walioshiriki katika kikao hicho, akiwemo Ndg. Stanley Gowele na Dominic Hule walieleza kuwa wamejipanga kikamilifu kutekeleza mradi huo na wameomba ushirikiano kutoka kwa uongozi wa halmashauri na wananchi ili kuhakikisha mradi huo unakuwa na tija kwa wote. “Tunaomba tushirikiane kwa pamoja ili kuongeza thamani ya mradi tunaokwenda kuutekeleza; tupo tayari kusaini mkataba na kuanza kazi mara moja,” alisema Gowele.
Zoezi la kusainishana mikataba lilihitimishwa kwa mafanikio chini ya usimamizi wa Mwanasheria Mkuu wa Halmashauri, Ndg. Mathan Chalamila, ambaye alihakikisha kuwa mikataba yote imesainiwa kwa kuzingatia taratibu na sheria zilizopo.
Mradi huu wa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya uvuvi katika Wilaya ya Ludewa, na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya kiuchumi ya wananchi na taifa kwa ujumla.