Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Hemed Challe (MNEC), ameendelea na ziara yake ya kikazi kwa siku ya pili katika Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma, akitembelea kata mbalimbali za Mbinga Vijijini na Mjini, huku akikutana na viongozi wa chama, wanachama, pamoja na wananchi kwa lengo la kuhamasisha maendeleo na mshikamano ndani ya CCM.
Katika ziara hiyo, MNEC Hemed amefanya mikutano ya hadhara kwenye kata mbalimbali ambapo amezungumza na viongozi wa kata, mabalozi na kamati zao, jumuiya zote za chama kuanzia ngazi ya matawi, pamoja na viongozi wa dini kwa lengo la kufikisha ujumbe wa amani kwa waumini wao, Wananchi pia walihudhuria mikutano hiyo kama sehemu muhimu ya utekelezaji wa demokrasia na maendeleo ya kijamii.
Akiwa katika Jimbo la Mbinga Mjini, Hemed Challe amekipatia Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Mbinga msaada wa shilingi milioni 1.075 kwa ajili ya ununuzi wa mifuko 50 ya saruji, inayotarajiwa kutumika katika ujenzi wa ofisi mpya ya chama, Ametumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wa CCM kwa jitihada zao za kuhakikisha chama kinakuwa na miundombinu ya kisasa inayoendana na mahitaji ya sasa.
Jana, ziara yake ilimfikisha katika Kata ya Mbangamao, Halmashauri ya Mji wa Mbinga, ambako alihutubia mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Parokia ya Mbangamao, Katika hotuba yake amesisitiza kuwa lengo kuu la ziara hiyo ni kuhamasisha chama na wanachama wake kuendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi. Alitoa wito kwa wanachama wa CCM kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia Juni 28, 2025.
Katika hatua nyingine, Hemed aliwapongeza wananchi wa Mbangamao kwa kunufaika na miradi mingi ya maendeleo ikiwemo sekta ya elimu, afya, na maji, amewasihi viongozi wa chama na wananchi kwa ujumla kuhakikisha wanamuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumpigia kura nyingi katika uchaguzi ujao ili aweze kuendeleza kasi ya maendeleo nchini na kuufanya Mkoa wa Ruvuma kuendelea kuvuma kiuchumi na kijamii.
Wakati wa mkutano huo, wananchi walimkabidhi MNEC Hemed ombi la kupewa rasmi mradi wa kituo cha afya na mradi wa maji, wakieleza kuwa vituo hivyo vitasaidia kupunguza adha ya kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma muhimu za afya, Walimshukuru pia Mbunge wao, Jonas Mbunda pamoja na Serikali ya Rais Samia kwa kuendelea kuwaletea maendeleo kupitia miradi hiyo.
Katika Kata ya Kitanda, Hemed aliwashukuru wananchi kwa mapokezi mazuri na kuwahimiza kuendeleza mshikamano, upendo na umoja miongoni mwa wanachama wa CCM, hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi, alisisitiza kuwa haki ya kugombea nafasi za uongozi ni ya kila mwanachama na hivyo ni muhimu kuepuka migawanyiko ndani ya chama.