-Una maneno yaliyotumiwa dhidi ya Nduli Idi Amin
-Asisitiza utaifa ulindwe kwa wivu mkubwa
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Emmanuel John Nchimbi amepiga marufuku wimbo unaobeza na kuchochea chuki dhidi ya vyama vya upinzani, akiagiza usitumiwe na wanaCCM popote, kwani wao wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kuhamasisha upendo, umoja na mshikamano nchini.
Balozi Nchimbi alichukua hatua hiyo alipokuwa akihutubia umati mkubwa wa maelfu ya wananchi wa Mji wa Shirati, wilayani Rorya, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Obwele, leo Ijumaa tarehe 25 Aprili 2025, akiwa katika siku ya nne ya ziara yake ya kikazi mkoani Mara.
Kabla ya kutoa kauli hiyo, kwanza Balozi Nchimbi aliwakumbusha wananchi waliokuwa wakimsikiliza wimbo maarufu uliokuwa unatumiwa na wanajeshi wa Tanzania kwenye Vita vya Kagera, wakati wa kumtoa na kumpiga Nduli Idi Amin Dada, aliyekuwa Rais wa Uganda, baada ya kuvamia mipaka ya Tanzania.
“Mnaukumbuka ule wimbo ulikuwa unaimbwa wakati wa Vita vya Kagera…Idi Amin akifa, mimi siwezi kulia, nitamtupa Kagera, awe chakula cha mamba…sasa naomba msikilize wimbo mwingine hapa, kisha niseme ninachotaka kukitolea kauli hapa,” alisema Balozi Nchimbi.
Akitumia simu yake kuucheza wimbo huo na kuwasikilizisha wananchi kupitia kipaza sauti alichokuwa anatumia kuhutubia, walisikika watu wakiimba wimbo unaofanana na ule wa dhidi ya Nduli Amin, huku wakiwa wamebadili maneno na kuweka mengine yanayolenga kubeza na kuchochea chuki dhidi ya vyama vya siasa vya upinzani nchini.
“Natumia nafasi hii kuendelea kusisitiza amani, umoja, mshikamano. Mwaka huu ni uchaguzi mkuu. Ni mwaka wenye vishawishi vingi. Ni lazima sana watu, hasa wanasiasa wapime kauli zao. Wawe wanasiasa wa CCM au vyama vingine, muhimu sana watoe kauli zenye kulenga kuimarisha utaifa wetu. Lazima tuulinde utaifa wetu kwa wivu mkubwa.
“Maneno haya katika wimbo huu ni maneno yanayojenga chuki. Hayajengi upendo. Napiga marufuku wimbo huu. Sisi wanaCCM tuna dhamana kubwa katika nchi hii. Lazima tuongoze kwa mfano. Tuunganishe watu. Tusiwe chanzo cha vurugu. CCM ndiyo baba na mama wa demokrasia nchini,” alisema Balozi Nchimbi kwa msisitizo.
Aidha, Balozi Nchimbi, mbali ya kutoa wito huo kwa wanaCCM, pia alitoa rai kwa viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani: “Wote, wanaCCM na vyama vya upinzani tujiepushe na kauli zinazochochea chuki na shari na vurugu. Hata tukimsikia kiongozi wa upinzani anatoa kauli za kuchochea, tuwatafute ndugu zake huko Singida, kuwa mshaurini ndugu yenu huko anakotupeleka siko.”
Kabla ya hapo, Balozi Nchimbi alitoa maelekezo kwa Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdalla Ulega, kuwahakikishia wananchi wa Rorya kwenye mkutano huo, kwa njia ya simu, kuhusu utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa Barabara ya Mika – Utegi – Shirati – Kirongwe yenye kilometa 56, ambayo tayari imeshatangazwa na itaanza kujengwa mwisho wa mwezi huu, mara tu baada ya mkandarasi kupatikana.