Ni kauli yake Mhe. Kasalali Emmanuel Mageni Mbunge wa Jimbo la Sumve Mkoa wa Mwanza, alipokuwa akichangia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yusph Masauni (Mb) aliyoiwasilisha leo kuhusu mapitio ya utekelezaji wa mpango na bajeti kwa mwaka 2024/2025 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2025/2026.
Amesema NEMC kama chombo chenye dhamana ya Mazingira nchini kinatakiwa kusimamia mazingira kwa misingi ya Sheria na kutoa maamuzi yasiyoingiliwa wala kupingwa na mtu yeyote.
“Tukizungumzia suala la kelele, wananchi wamekuwa wakiteseka, mabaa yamejaa kila kona, bila kujali vibali vya maeneo husika, NEMC wakifungia, mamlaka nyingine zinakuja zinafungua, kwa hiyo inakuwa ni ngumu kusimamia utekelezaji wake”
Amesema mazingira yanaendelea kuharibiwa na shughuli za kibinadamu kutokana na kukosekana kwa mamlaka yenye nguvu ya kuchukua hatua kwa wanaoendelea kuharibu mazingira.
Awali akiwasilisha hotuba ya mapitio ya utekelezaji wa mpango na bajeti kwa mwaka 2024/205 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2025/2026 Mhandisi Hamad Masauni (Mb) amesema Baraza litaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, sura 191 kwa kuendelea kutekeleza sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021.
Kadhalika itaendelea kutekeleza mkakati wa Taifa wa matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034), kuendelea kuratibu mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira, kusajili wataalam elekezi wa Mazingira na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya hifadhi na usimamizi wa mazingira.