NA WILLIUM PAUL, HAI.
MKUU wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amewataka wananchi mkoani humu kuendelea kuuenzi, kuudumisha na kuulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kutowapa nafasi baadhi ya watu wenye chokochoko ya kutaka kutia maneno ya chuki kuhusu Muungano.
Babu alitoa kauli hiyo leo alipokuwa akiwahutubia Wananchi wa kijiji cha Mkalama kata ya Rundugai wilayani Hai mkoani Kilimanjaro ambapo maadhimisho hayo yalifanyika kimkoa kwa kupanda miti 15000 katika eneo la uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na badae kuzungumza na wananchi.
Alisema kuwa, muungano huo umepelekea Wananchi kutoka Tanzania bara kwenda Zanzibar kifua mbele huku wengine wakitoka Zanzabar kuja Tanzania bara kifua mbele ambalo yote hayo yamechangiwa na uwepo wa muungano huo.
“Watanzania bara wengi wapo Zanzibar wanapata elimu na wapo Wazanzibar wanapata elimu kwenye vyuo vikuu na vyuo vingine kwa uhuru na upendo mkubwa kwa sababu ya tunu ya muungano wetu hivyo Wanakilimanjaro tunawajibu wa kuendelea kuulinda muungano” alisema Babu.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa, viongozi wameweza kuwaweka wananchi pamoja na kuhakikisha dosari za muungano zilizokuwa zinasemwa zimetatuliwa ambapo kwa sasa zimebaki tatu ambapo nazo zinafanyiwa kazi.