Ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake mjini Songea, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC) kutoka Mkoa wa Ruvuma, Hemed Challe, ameendelea na mikutano yake ya kuwafikia wananchi na kujionea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na wakazi wa Kata saba za Ruvuma, Subira, Majengo, Mjini, Bombambili, Mfaranyaki na Misufini kwa nyakati tofauti, MNEC Hemed alisema kuwa ziara yake imebainisha wazi namna serikali ya CCM imewekeza kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa miradi ya jamii, ikiwemo sekta ya afya, elimu, barabara, pamoja na huduma nyingine muhimu zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
“Mafanikio haya yanadhihirisha dhamira ya dhati ya CCM katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli, kwa kupeleka fedha nyingi kwenye miradi ya kijamii ili kuhakikisha huduma bora zinafika kila kona ya nchi,” alisema MNEC Hemed.
Katika mazungumzo yake, alieleza kuwa CCM imeendelea kushika dola kwa kuzingatia misingi ya kidemokrasia, jambo ambalo limeiwezesha kuendelea kuaminiwa na wananchi, Alifafanua kuwa ni nadra sana katika mataifa mengi kukuta chama kilichopigania uhuru bado kikiwa madarakani, tofauti na CCM ambayo imejijengea imani kwa kuzingatia matakwa na mahitaji ya wananchi wake.
Akiwa katika kata mbalimbali, MNEC Hemed aligusia pia changamoto zinazowakabili wananchi, akisema kuwa si rahisi kuzitatua zote kwa wakati mmoja, lakini serikali kupitia CCM itaendelea kuzitatua hatua kwa hatua. Alitoa mfano wa Kituo cha Afya Ruvuma ambacho kwa sasa kimeanza kutoa huduma, hali ambayo imepunguza adha kwa wananchi waliokuwa wakikosa huduma hizo awali.
Aidha, alisisitiza kuwa nafasi zote za uongozi si za kudumu na kila mwananchi ana haki ya kugombea pale uchaguzi unapofika, kwa mujibu wa katiba. Aliwahamasisha wananchi wanaojisikia kuwa na uwezo wa kuongoza, kujitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi za udiwani au ubunge pindi muda utakapowadia.
Katika kuunga mkono juhudi za chama, MNEC Hemed alichangia jumla ya Shilingi Milioni Tatu: Milioni Moja kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za CCM Kata ya Ruvuma, Milioni Moja kwa ofisi ya CCM Misufini, na Milioni Moja nyingine kwa ajili ya kununua samani katika ofisi ya CCM Kata ya Bombambili. Vilevile, alitoa misaada ya kilo 50 za sukari kwa jumuiya ya Wazazi Kata ya Subira (mtaa wa Liwena), vifaa vya ujenzi kwa ofisi ya tawi la CCM Mahenge (Kata ya Mjini), pamoja na jezi na mipira kwa UVCCM katika Kata zote saba alizotembelea.
Katibu wa CCM Wilaya ya Songea Mjini, James Mgego, alitoa pongezi kwa MNEC Hemed kwa kufanikisha ziara hiyo, akisema kuwa chama na wananchi kwa ujumla wameipokea kwa moyo mmoja, Aliongeza kuwa mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa, jambo linaloonyesha mshikamano na imani waliyonayo kwa CCM na viongozi wake. Aidha, aliahidi kuwa CCM Songea Mjini itahakikisha haki na uwazi katika mchakato wa uchaguzi ujao.
Ziara ya MNEC Hemed ilianza katika Wilaya ya Nyasa, kisha Mbinga Mji na Mbinga Vijijini, kabla ya kuingia rasmi mjini Songea hapo jana, Hadi hivi sasa, Takribani Kata 13 zimefikiwa, huku akitarajia kukamilisha ziara hiyo kesho Aprili 28 kwa kutembelea maeneo yaliyosalia kwa mpangilio uliozingatia jiografia ya maeneo husika.