Na Diana Byera – Missenyi
Kampeini ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia wilayani Missenyi Mkoani Kagera, imefanikiwa kwa asilimia 95.3 ndani ya siku 15 tangu ilipozinduliwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, Aprili 14 mwaka huu katika viwanja vya Mayunga, Manispaa ya Bukoba.
Mratibu wa kampeini hiyo wilayani Missenyi Maxmillan Fransis, alisema kuwa ndani ya siku hizo 15, kuanzia Aprili 15 hadi Aprili 28, kata zote 15 zilizopangwa kufikiwa zimefikiwa, na vijiji 43 vilivyopangwa kufikiwa, 41 vilifikwa.
“Kampeini imekuwa na mafanikio makubwa na mwitikio mkubwa sana. Mwanzoni ilipangwa iwe ya siku 10, lakini serikali iliongeza siku 5 kulingana na uhitaji wa wananchi, Tumefikia vijiji 41, na vijiji viwili ambavyo kampeini haikufanikiwa, tulifika lakini viongozi walisema wana misiba mikubwa. Vingine vyote vimenufaika na kampeini hiyo,” alisema.
Aliongeza kuwa kupitia kampeni hiyo, makundi mbalimbali yalipata elimu, yakiwemo ya bodaboda, wanafunzi, wakulima, wazee, watu wenye ulemavu, taasisi binafsi, waajiriwa serikalini, huku elimu kuhusu umiliki wa ardhi, matumizi sahihi ya ardhi, wosia, mirathi, ukatili na matunzo ya watoto ikitolewa katika mikutano ya hadhara ili kunufaisha umma na kuwafundisha kufuata sheria.
Alisema kuwa migogoro iliyojitokeza kwa wingi ni ya ardhi, mirathi na ukatili, ambapo mingi imetatuliwa kwa njia ya usuluhishi. Migogoro ambayo haijatatuliwa imekabidhiwa kwa vitengo husika ili kupata utatuzi wa kudumu.
Aidha, migogoro ya kisheria kwa wananchi ambao hawana mawakili, tayari mashauri yao yamekabidhiwa kwa mawakili ili kuwasaidia kuendelea na hatua za mahakama.
Akitaja mafanikio yaliyopatikana, alisema kuwa elimu ya masuala ya kisheria imetolewa na kufikia wananchi 14,020, ambapo wanaume ni 6,905 na wanawake ni 7,115.
Aidha, watendaji wa vijiji, kata, wenyeviti wa vijiji na vitongoji pamoja na madiwani wamejengewa uwezo juu ya masuala ya kisheria kutokana na kushughulikia kero za wananchi kila siku, ambazo zinahitaji utaalamu wa masuala ya kisheria.
Changamoto zilizojitokeza ni pamoja na uwepo wa malalamiko ya muda mrefu kuhusu matumizi ya ardhi baina ya wananchi na serikali za vijiji, jambo ambalo limechochea uvunjifu wa amani na baadhi ya wananchi kugoma kuchangia maendeleo ya vijiji kwa sababu ya migogoro ya ardhi.