Mkuu wa Kitengo cha Usalama wa Miundombinu Muhimu Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Richard Ngole kutoka Makao Makuu ya Polisi Dodoma amekagua mazingira ya kiulinzi ikiwa ni pamoja na mifumo ya Operesheni ya kamera za kisasa za Kiusalama (CCTV CAMERA) iliyopo katika mgodi wa Anglo Songwe uliopo Kijiji cha Patamela Wilaya ya Songwe.
SACP Ngole amefanya ukaguzi huo Mei 10, 2025 na kuwapongeza viongozi waandamizi wa mgodi huo kwa namna ambavyo wamelipa kipaumbele suala la ulinzi kwa kufunga kamera za kisasa ili kubaini na kutanzua uhalifu na wahalifu katika eneo hilo kwa lengo la kufanya shughuli za uzalishaji katika hali ya usalama.
Pamoja na mambo mengine, SACP Ngole alifanya kikao na baadhi ya wafanyakazi pamoja na viongozi waandamizi wa mgodi huo na kuwataka kufanya kazi kwa nidhamu wakati wote sambamba na kutoa huduma bora kwa wananchi wakishirikiana na Jeshi la Polisi ili kuendelea kukuza uchumi wa nchi.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Mgodi huo Yasin Rashid alisema kuwa wataendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kuendelea kuweka mifumo ya kisasa zaidi hasa katika idara ya usalama katika mgodi huo ikiwa na lengo la kuimarisha mazingira bora ya kazi na kulinda rasilimali za mgodi kwa maendeleo ya kampuni hiyo na ukuaji wa uchumi wa nchi.