-Wakubaliana kuanzishwa kwa Jukwaa la Wafanyabiashara
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na Waziri Mkuu wa Côte d’Ivoire, Robert Beugre Mambe na kujadiliana naye masuala ya kidiplomasia, kiuchumi, teknolojia, kilimo na michezo kwenye kikao kilichofanyika ofisini kwa mwenyeji wake, Boulevard Angoulvant Plateau, jijini Abidjan.
Akitoa ufafanuzi mara baada ya kikao hicho jana jioni (Jumanne, Mei 13, 2025), Waziri Mkuu Majaliwa alisema lengo la kikao chao lilikuwa kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia lakini pia kuhimiza haja ya nchi hiyo kushirikiana na Tanzania kwenye masuala mbalimbali ikiwemo utafiti na teknolojia za kisasa kwenye kilimo.
“Côte d’Ivoire ina wakazi zaidi ya milioni 31 na inaongoza kwa kilimo cha kakao, korosho na michikichi. Hawa wanalima korosho zaidi kuliko Tanzania, na sisi tunalima korosho kwenye mikoa ya Pwani na kakao kule Mbeya na maeneo mengine. Tunaweza kujifunza kwao na sisi tunaiona hii ni fursa kwetu ya kuongeza uzalishaji kwenye mazao haya.”
“Kakao ni zao kuu la biashara na linawaingiza fedha nyingi za kigeni. Tumekubaliana kuwa mawaziri wetu wa kilimo wakutane na waangalie ni maeneo gani ya kuweka mikataba ikiwemo utafutaji wa masoko na masuala ya utafiti,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa ambaye alikuwa Abidjan kumwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika jukwaa la siku mbili la Maafisa Watendaji Wakuu barani Afrika lililomalizika jana.
Alisema mazungumzo yao yamefungua milango ya kuimarisha biashara na wamekubaliana na mwenyeji wake kwamba mawaziri wa nchi hizo wa viwanda na biashara pamoja na wa mambo ya nje wakutane na kuweka ajenda ya kwanza ya kufanyika kwa Jukwaa la Kibiashara baina ya Tanzania na Côte d’Ivoire.
“Tumekubaliana kuwa jukwaa hilo lifanyike mapema ili wafanyabiashara wetu wakutane na kubadilishana mbinu na hapa tunataka sekta binafsi ilisimamie eneo hilo. “Kupitia TPSF, taasisi zikae pamoja na kuainisha ni maeneo yapi ya kujengeana uwezo, iwe ni teknolojia mpya au ubadilishanaji wa wawekezaji katika mazao ya kokoa na korosho.”
“Tumewahakikishia kuwa tumepunguza muda wa kupata leseni nchini, tumeongeza maeneo ya uwekezaji (EPZA) na hivi karibuni tunatarajia kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kuja Côte d’Ivoire na Nigeria. Tunataraji hatua hiyo itaongeza masoko lakini pia itakuza utalii,” alisema.
Mapema, Waziri Mkuu wa Côte d’Ivoire, Robert Beugre Mambe ambaye pia ni Waziri wa Michezo na Ustawi wa Jamii, alimshukuru Waziri Mkuu kwa kushiriki mkutano huo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye alisema anatambua kwamba ana majukumu mengine ya kitaifa.
Alisema anampongeza Mheshimiwa Rais wa Tanzania kwa hatua kubwa aliyofikia katika kuiongoza Tanzania huku akiipongeza Tanzania kwa kuandaa mkutano mkubwa wa nishati Afrika uliofanyika Januari 27 -28, mwaka huu.
Alisema anakubaliana na mambo waliyojadiliana leo kwenye masuala ya kilimo cha kakao,korosho na michikichi na kwamba wako tayari kushirikiana na Tanzania kwenye shughuli mbalimbali kadri zitakavyopangwa.
“Tunataraji kushirikiana nanyi kwenye masuala ya zana za kisasa za kilimo. Teknolojia ya kilimo huku kwetu iko juu sana na tunasubiri kuanza kwa jukwaa la wafanyabiashara ili watu wetu waweze kubadilishana uzoefu,” alisema.