Katika azima ya ushirikiano wa Mamlaka za Usimamizi wa Masoko ya Mitaji Afrika Mashariki (EASRA), Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewezesha wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Masoko ya Mitaji (ARMC) na wataalamu wa masoko ya mitaji kutoka Jamhuri ya Burundi kushiriki kwa mafanikio kwenye programu ya mafunzo ya wiki sita ya taaluma katika masoko ya mitaji.
Mafunzo hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania, chini ya uratibu wa CMSA kupitia programu inayotambuliwa na Taasisi ya Chartered Institute for Securities and Investment (CISI) ya Uingereza. Programu hiyo imewapatia watu 29 alama ya umahiri na uadilifu wa kitaaluma, na hivyo kuwapa sifa za kutoa huduma katika masoko ya mitaji ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki na kimataifa.
Akizungumzia maendeleo hayo ya kihistoria, Afisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, CPA. Nicodemus Mkama alisema “juhudi hizi ni sehemu ya ajenda pana ya ujumuishaji wa kikanda chini ya EASRA na zinadhihirisha maono ya pamoja kati ya CMSA na ARMC ya kuunda nguvu kazi yenye maarifa, ujuzi na maadili katika sekta ya masoko ya mitaji ambayo itachangia katika ukuaji wa uchumi endelevu wa ukanda huu.
Kupitia kozi ya Mafunzo ya Kitaalamu ya Sekta ya Dhamana, tunalenga kuongeza uwezo wa wataalamu wa masoko ya mitaji ili kuendana na maendeleo yanayoendelea kwenye masoko ya mitaji duniani.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ARMC, Dkt. Arsene Mugenzi alisema, “juhudi hii ya kuendeleza uwezo itaiwezesha ARMC kujenga msingi imara wa kukuza tasnia changa ya masoko ya mitaji nchini Burundi. Pia, inaiwezesha ARMC kuendana na azma za EASRA katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kuinua viwango vya taaluma, na kuendeleza masoko ya mitaji yenye nguvu na yaliyo na usimamizi thabiti katika Afrika Mashariki.”
Jumla ya washiriki 93 walifuzu mafunzo, wakiwemo washiriki 29 kutoka Burundi. CMSA na ARMC zote zimethibitisha dhamira yao ya kuendeleza ushirikiano katika nyanja za kujenga uwezo, kuoanisha kanuni za udhibiti, na kukuza masoko ya mitaji kwa ajili ya ukuaji na mtangamano wa masoko ya mitaji Afrika Mashariki.