Bodi ya Maji ya Bonde la Wami/Ruvu – Kidakio cha Pwani imefanya kikao kazi maalum na kamati ya Mazingira kikihusisha wadau mbalimbali wakiwemo wataalamu wa mazingira, viongozi wa mitaa na kamati za mazingira. Lengo kuu la kikao hicho ni kuratibu na kupanga mikakati ya usafishaji wa Mto Mpiji na mito mingine katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuzingatia kanuni za kitaalamu na uhifadhi wa mazingira.
Katika kikao hicho, washiriki walikubaliana kwamba usafishaji wa mito lazima uendane na utunzaji wa ikolojia kwa kuondoa taka, tope na mchanga bila kuathiri mazingira ya asili. Aidha, walisisitiza umuhimu wa kulinda kingo za mito na kudhibiti mafuriko sambamba na kuimarisha ajira kwa vijana kupitia shughuli hizo.
Kikao pia kimejadili suala la ukusanyaji wa kodi na mirabaha kwa wachimbaji wa mchanga ili mapato hayo yatumike kuboresha mazingira. Hata hivyo, changamoto kadhaa zimeibuliwa zikiwemo ukwepaji wa tozo za kisheria na uchimbaji usiozingatia sheria pamoja na ukosefu wa ushirikiano wa kutosha kati ya wadau.
Mhandisi Diana Kimbute, Mkuu wa Ofisi ya Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu – Kidakio cha Pwani, amehimiza wataalamu kushiriki kikamilifu katika maamuzi, kudhibiti ujenzi holela ndani ya mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji na kuimarisha mawasiliano kati ya wadau wote. Alisisitiza kuwa mafanikio ya juhudi hizi yanategemea mshikamano na uwajibikaji wa pamoja kwa ajili ya mustakabali wa mazingira ya Jiji la Dar es Salaam.