Kupitia Mradi wa Digital Tanzania, taasisi za umma na binafsi haziitaji tena kuwekeza kwenye mifumo yao binafsi, bali zinahimizwa kuwekeza katika Kituo cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC) ambacho kinatoa huduma kwa gharama nafuu na kwa usalama wa uhakika.
Akizungumza baada ziara ya Mhe. Kassim Majaliwa(Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alipotembelea Kituo cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC) kwa lengo la kuangalia Mfum wa N- CARD unavyofanya kazi,Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Slaa, alisema Serikali imejipanga kuhakikisha mifumo yote inasomana kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi kupitia Mradi wa Digital Tanzania.
Kadi hiyo itarahisisha miamala ya kifedha na itatumika katika huduma mbalimbali kama vile viingilio vya viwanja vya mpira, vivuko, usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka (UDART), taasisi za kifedha na maeneo mengine ya muhimu.
“Mradi wa Digital Tanzania ambao ni sehemu ya utekelezaji wa Kadi Jamii unaendelea kutekelezwa kwa lengo la kuhakikisha mifumo yote ya taasisi mbalimbali inasomana, ili kuwezesha utoaji wa huduma kwa ufanisi,” alisema Waziri Slaa.
Ameeleza kuwa katika bajeti ya mwaka 2024/2025, serikali ilitenga Shilingi bilioni 10 kuiwezesha NIDC kuimarisha huduma zake, zikiwemo zinazotekelezwa kupitia mradi huo wa kidijitali.
Kupitia mradi huu, wananchi wataweza kutumia Kadi Jamii yenye kuunganishwa na namba yao ya NIDA kufanya miamala yote ya kifedha na manunuzi, hivyo kuondoa hitaji la kubeba kadi nyingi.
Waziri Slaa alisema hatua hiyo inalenga kumrahisishia mwananchi maisha ya kila siku kwa kumwezesha kutumia kadi moja tu kwa huduma mbalimbali, na kwamba serikali ipo kwenye mkakati wa kuhakikisha kila mwananchi anamiliki simu janja kwa gharama nafuu ili kuitumia sambamba na kadi hiyo.
Aidha, alieleza kuwa Mkongo wa Taifa unaosimamiwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) tayari umeunganisha wilaya 109 kati ya 139 na baadhi ya nchi jirani za Afrika zimeunganishwa na mkongo huo, hatua ambayo itaongeza ufanisi na kupanua huduma za kidijitali nchini.