Arusha 16 Mei 2025 – Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, amezindua rasmi Shule ya Sekondari ya Mfano ya Benki ya CRDB, itayojengwa katika Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya Benki ya CRDB.
Shule hiyo ya kisasa ni matokeo ya dhamira ya Benki hiyo ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwekeza kwenye elimu bora kwa watoto wa Kitanzania.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa shule hiyo uliofanyika katika seimna ya wanahisa wa Benki ya CRDB kuelekea Mkutano Mkuu, Dkt. Mpango aliipongeza Benki ya CRDB kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya kijamii, hususan sekta ya elimu.
“Nawapongeza kwa kuwa mfano wa kuigwa kwa sekta binafsi. Mmekuwa mstari wa mbele sio tu kwenye huduma za kifedha bali pia katika kuleta mabadiliko ya kweli kwenye jamii,” alisema Dkt. Mpango huku akiipongeza benki hiyo pia kwa kutimiza miaka 30 tokea kuanzishwa kwake mwaka 1996.
Akizungumza katika semina hiyo ya wanahisa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay, tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996, Benki ya CRDB imeendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo kwa Taifa kwa kutoa huduma za kifedha zenye kugusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Shule ya Sekondari ya Mfano ya Benki ya CRDB ina uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 600 na imejengwa kwa viwango vya kisasa ikiwa na madarasa ya kisasa 16, maabara 4, maktaba 1 chumba cha TEHAMA 1, ofisi za walimu na wafanyakazi 11, vyoo 53, miundombinu rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, pamoja na maeneo rafiki ya michezo. Mradi huu unatarajiwa kugharimu takribani shilingi bilioni 5.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Mussa Nsekela, alisema shule hiyo ni zawadi ya Benki kwa Watanzania katika kuadhimisha miaka 30 ya mafanikio ya benki hiyo. “Tulipojiuliza ni zawadi gani ya kipekee tungeweza kuwapa Watanzania katika kutimiza miaka 30, tulikubaliana kwamba elimu ni urithi wenye nguvu kuliko wote. Shule hii ni ushahidi wa dhamira yetu ya kuwekeza katika kizazi kijacho,” alisema Nsekela.
Nsekela aliongeza kuwa shule hiyo ni sehemu ya mpango mpana wa Benki ya CRDB wa kurudisha kwa jamii katika nyanja za ya elimu, afya, mazingira na uwezeshaji wanawake kupitia CRDB Bank Foundation. “Tunaamini kuwa maendeleo endelevu hayawezi kufikiwa bila uwekezaji wa makusudi katika elimu. Kupitia shule hii, tunaweka msingi wa taifa lenye maarifa, maadili na ushindani wa kimataifa,” alibainisha.
Akitoa salamu zake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb), aliishukuru Benki ya CRDB kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya sekta ya elimu nchini. “Kwa niaba ya Serikali na Wizara ya Elimu, naishukuru sana Benki ya CRDB kwa maono na uamuzi huu wa kujenga shule ya kisasa kwa ajili ya watoto wa Kitanzania. Huu ni mfano hai wa jinsi sekta binafsi inavyoweza kushirikiana na Serikali katika kujenga musatakabali bora kwa watoto na vijana wetu.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CRDB Bank Foundation, Martin Warioba, alisema shule hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa Benki ya CRDB kuboresha mazingira ya elimu nchini na kufungua fursa kwa watoto wa Kitanzania. “Mbali na kujenga shule hii ya mfano, tumejipanga pia kuanzisha mpango wa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi kwa kushirikiana na Wizara ya elimu.”
Uzinduzi wa shule hiyo unachukuliwa kama alama ya mafanikio ya miaka 30 ya Benki ya CRDB, na uthibitisho wa maono yake ya kujenga taifa lenye misingi imara ya elimu, usawa na maendeleo endelevu. “Tunajivunia kuona uwekezaji wetu ukiendelea kuzaa faida zaidi katika jamii,” alisema mmoja ya Wanahisa waliohudhuria semina hiyo.
Wanahisa wa Benki ya CRDB watafanya Mkutano Mkuu wa 30 kesho ambapo ajenda mbalimbali zinatarajiwa kujadiliwa ikiwamo kuidhinisha pendekezo la bodi ya wakurugenzi la gawio la shilingi 65 kwa hisa ikiwa ni ongezeko la asilimia 30 kulinganisha na gawio la shilingi 50 kwa hisa lililotolewa kwa mwaka 2023.