.jpeg)
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Eng. Yahya Samamba akizungumza jijini Dar es Salaam leo Mei 16, 2025 katika uzinduzi wa Kamati ya Masoko na Mawasiliano ya TAMISA.

Katibu wa TAMISA, Dkt. Theresia Numbi akizungumza katika uzinduzi wa Kamati ya Masoko na Mawasiliano ya TAMISA lililofanyika jijini Dar es Salaam leo Mei 16, 2025.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano na Masoko ya Chama cha Wasambazaji wa Huduma katika Sekta ya Madini Tanzania (TAMISA), Dkt. Sebastian Ndege akifafanua jambo wakati wa kongamano la TAMISA lililofanyika jijini Dar es Salaam leo Mei 16, 2025.
SERIKALI kupitia Wizara ya Madini imeitaka Chama cha Wasambazaji wa Huduma katika Sekta ya Madini Tanzania (TAMISA) kusimamia kwa weledi na uadilifu shughuli zote za sekta ya madini nchini ili kuhakikisha rasilimali hizo zinawanufaisha Watanzania, hususan wazawa.
Hayo ameyasemaleo Mei 16, 2025, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Eng. Yahya Samamba wakati akizungumza katika uzinduzi wa Kamati ya Masoko na Mawasiliano ya TAMISA, alisema kuwa Tanzania kwa sasa ina zaidi ya masoko 40 na vituo zaidi ya 100 vya kuuzia madini, jambo linaloonesha mafanikio makubwa ya sekta hiyo.
Eng. Samamba alisisitiza kuwa mafanikio haya yatakuwa na tija endapo TAMISA itasimamia ipasavyo shughuli zinazofanywa na wazawa, sambamba na kutekeleza maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Madini ya kuhakikisha uchimbaji na usambazaji wa madini unaleta faida kwa taifa.
“Tunapokusanya kodi pamoja na tozo zisizo za kikodi, hiyo ni hatua nzuri, lakini tukiweka nguvu zote katika ukusanyaji wa kodi bila kusimamia vizuri shughuli nzima ya sekta hii, manufaa halisi tutayaona baadaye tu baada ya Mwenyezi Mungu kutuwezesha kuwa na madini haya,” alisema Eng. Samamba.
Aidha, alieleza kuwa mabadiliko ya sheria na kanuni za sekta ya madini lazima yalenge kuwawezesha na kuwanufaisha wazawa, kwa kutoa ajira, mafunzo na kutumia teknolojia ya kisasa ili kuinua uwezo wa Watanzania kushiriki kikamilifu kwenye uchumi wa madini.
Amewataka TAMISA na wadau wake kuhakikisha wanazingatia masuala ya Local Content, ajira kwa vijana, pamoja na usimamizi wa teknolojia kwa maendeleo ya nchi.
“Serikali imedhamiria kuhakikisha vijana wanapata ajira kupitia sekta hii, na hilo litawezekana tu ikiwa sheria zitasimamiwa ipasavyo,” aliongeza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TAMISA, Peter Kumalilwa, alisema wamekuwa wakipokea malalamiko kutoka kwa wazawa kuhusu kupewa kazi na kushindwa kuzifanya kwa viwango stahiki, hali inayochangia ukosefu wa uaminifu na migogoro katika sekta hiyo.
“Tumejipanga kufanya tathmini ya kina ili kuongeza uaminifu na kupunguza migogoro,” alisema Kumalilwa.
Aliitaka serikali kutekeleza ahadi ya kuishirikisha TAMISA moja kwa moja kwenye zabuni za serikali, kama ilivyoahidiwa katika kikao cha Mei 1, 2025, jijini Dodoma.
“Ushirikishwaji huu utasaidia wanachama wetu kujiandaa mapema na kuchukua hatua stahiki ili kushiriki kikamilifu katika zabuni hizo,” aliongeza.
Aidha, alitaja changamoto ya wageni kupewa kazi ambazo kisheria ni za wazawa, akiiomba serikali kuingilia kati na kuhakikisha ushirikiano kati ya wageni na wazawa unazingatia sheria za Local Content ili kulinda maslahi ya wazawa na kuleta tija kwa taifa.
Katibu wa TAMISA, Dkt. Theresia Numbi, alieleza kuwa kuanzishwa kwa kamati maalum ya mawasiliano na masoko ni hatua ya kimkakati katika kusimamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali katika sekta ya madini na sekta nyingine za kiuchumi.
Alisema TAMISA ni matokeo ya kikao kati ya Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, na wadau wa sekta ya madini kilichofanyika Januari 2024, ambapo ilielekezwa kuanzishwa kwa chombo kitakachowaunganisha watoa huduma na wamiliki wa leseni nchini.
“Kuwepo kwa jukwaa la pamoja kutasaidia kuwashirikisha Watanzania katika sekta ya madini na kuhakikisha kipaumbele kinatolewa kwa bidhaa na huduma za wazawa,” alisema Dkt. Numbi.
Aliongeza kuwa usimamizi wa sheria na ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta hiyo umechochea fursa nyingi ikiwemo ajira, mafunzo, utafiti, uhamishaji wa teknolojia na manunuzi ya bidhaa zinazozalishwa nchini.
“Niwataarifu Watanzania mliopo hapa kuwa fursa za kwenye migodi ni kwa ajili yetu sote Watanzania,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Sekta Binafsi, Raphael Maganga, alisema kuwa uzinduzi wa kamati hiyo una lengo la kuhakikisha sekta binafsi inakuwa na ushawishi mkubwa katika uchumi wa Tanzania kupitia madini.
“Tunataka sera zetu ziwezeshe sekta binafsi kufikia malengo. Lengo letu ni kuhakikisha sekta ya madini inazalisha mabilionea wa kutosha nchini,” alisema Maganga.
Mkutano huo umeonyesha dhamira ya serikali na wadau wa sekta ya madini kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha sekta hiyo inachangia kwa kiwango kikubwa katika maendeleo ya taifa kwa kuwezesha wazawa kushiriki kikamilifu.
Matukio mbalimbali wakati wa kongamano la TAMISA lililofanyika leo Mei 16, 2025 jijini Dar es Salaam.
Picha ya pamoja.