SERIKALI ya Tanzania imeendelea kupata pongezi kutoka kwa
wawekezaji wa kigeni kwa jitihada zake za kuboresha mazingira ya biashara,
ikiwemo kurahisisha taratibu za usajili wa kampuni na kuwapa wawekezaji fursa
ya kuanza shughuli haraka bila vikwazo vikubwa vya kiutendaji.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi
wa tawi jipya la Kampuni ya Teknolojia ya Spidd Africa nchini, Meneja wa
Maendeleo ya Biashara wa kampuni hiyo, Catherine Kisaka, amesema Tanzania
imeonesha dhamira ya dhati ya kuvutia wawekezaji kupitia sheria rafiki na
mifumo ya kidijitali inayowezesha usajili wa haraka wa kampuni.
Ameeleza kwamba Spidd Africa, kampuni yenye makao makuu
nchini Uganda, inalenga kuleta mageuzi ya kidijitali katika sekta ya biashara
barani Afrika kupitia suluhisho bunifu, hususani kwa wajasiriamali wadogo,
biashara za kati, na mashirika makubwa.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Spidd Afrika kutoka Uganda,
Angela Semwogerere, amebainisha kwamba moja ya malengo makuu ya kampuni hiyo ni
kutoa elimu na mafunzo kuhusu usalama wa kimtandao kwa taasisi mbalimbali, ili
kuongeza uelewa na ulinzi wa taarifa katika ulimwengu wa kidijitali.
Kufunguliwa kwa tawi la Spidd Africa nchini kunatarajiwa
kuchochea mabadiliko chanya katika sekta ya teknolojia ya habari na
mawasiliano, pamoja na kukuza ajira na ubunifu kwa vijana wa Kitanzania.