NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
THAMANI ya shilingi imetajwa kuimarika huku ukwasi katika soko la fedha za kigeni ukiongezeka, wastani wa siku kwa mwezi mmoja ambapo ukwasi wa dola reja reja umeongezeka kutoka dola za kimarekani milioni 40 mpaka 69 .
Hii ni baada ya kuanza kwa utekelezwaji wa kanuni za matumizi ya fedha za kigeni juu ya bei na malipo ya bidhaa na huduma ndani ya nchi kufanyika kwa shilingi.
Ameyasema hayo leo Mei 20, 2025 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Akaro wakati wa Semina ya waandishi wa habari iliyofanyika katika ukumbi wa BoT.
Aidha Akaro mesema waliokuwa wanatumia fedha za kigeni kufanya miamala moja kwa moja kwa sasa wanakwenda sokoni kubadilisha na kulipa kwa shilingi na kuleta manufaa ya shilingi ya Tanzania kuwa himilivu ukilinganisha na vipindi vya nyuma.
Akaro amesema mwaka huu fedha za kigeni zilizoko katika soko zimeongezeka ukilinganisha mwaka jana kipindi kama hiki tulikuwa na dola za kimarekani milioni 30 kwa siku na sasa ni takribani dola za kimarekani milioni 70.
“Sera za BoT ndio zitakuwa zinatumika katika kuhakikisha mategemeo ya mfumuko wa bei yanasimamiwa vizuri na mfumuko wa bei unaendelea kuwa tulivu kwa asilimia 3.1,” Amesema Akaro.
Amesema kuwa mwaka huu wameshatoa fedha za kigeni dola za kimarekani milioni 130 na mwaka jana walitoa nyingi sokoni kuhakikisha shilingi inaendelea kuimarika, hivyo kila anayehusika kuhakikisha miamala yote inafanyika ndani ya nchi ifanyike kwa shilingi na inayofanyika nje itumie fedha za kigeni.
Machi 28, mwaka huu, serikali kupitia Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba ilitoa kanuni zinazohusiana na katazo la matumizi ya fedha za kigeni ndani ya nchi yetu kufanya miamala ya bidhaa na huduma hivyo katika katazo hilo wananchi hawaruhusiwi kutumia sarafu ya kigeni katika kufanya manunuzi ya bidhaa na huduma ndani ya nchi.
Kanuni za Matumizi ya Fedha za Kigeni, GN. Na. 198 ya mwaka 2025, zilizotungwa chini ya Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, Sura ya 197, zilichapishwa Machi 28, 2025 huku zinawahusu watu binafsi na wafanyabiashara wote nchini.