Mkuu wa mkoa wa Arusha Paul Makonda akizungumzia kuhusiana na daftari hilo .
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda leo Jumanne Mei 20, 2025 ameungana na Watanzania wengine kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kwenye kituo cha Hospitali ya AICC, Mtaa wa Mahakama Kata ya Sekei Jijini Arusha.
Mara baada ya kujiandikisha, Mhe. Makonda akizungumza na wanahabari amewasihi wananchi wa Mkoa wa Arusha kujitokeza kwa wingi kuhuisha taarifa zao katika vituo vilivyoainishwa ili waweze kupata haki ya msingi ya kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
“Mimi nilikuwa naishi Dar es Salaam, nimehamia hapa Arusha kwahiyo nimehamisha taarifa zangu rasmi za kutoka Dar es Salaam Mikocheni kwenye kituo cha Kontena kuja hapa kituo cha mahakamani, hivyo mimi ni mpiga kura halali wa Mkoa wa Arusha, Jimbo la Arusha Mjini, Kata ya Sekei.” Amesema Mhe. Makonda.
Katika hatua nyingine Mhe. Makonda amewataka waajiri wote katika Mkoa huo kutoa ruhusa kwa watumishi wa Umma, Mashirika na Taasisi mbalimbali kwenda kuhuisha taarifa zao kwa kuwa zoezi hilo halichukui muda mrefu kukamilisha taarifa za mpiga kura ili nao waweze kupata haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi watakaowaongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Mkoa wa Arusha una jumla ya vituo 331 kwaajili ya kuhuisha taarifa za wapiga kura ili kusaidia kuondoa usumbufu wakati wa kupiga kura na zoezi hilo litahitimishwa kwa mara ya pili tarehe 22 Mei, 2025.




