Zanzibar imechukua hatua madhubuti katika kujenga mazingira bora ya uwekezaji wa kimataifa kupitia uchumi wa buluu, huku Equity Bank Tanzania ikijitokeza kama daraja muhimu kati ya visiwa hivyo na jumuiya ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Hii ni sehemu ya jitihada za kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha biashara na maendeleo endelevu.
Katika Jukwaa la Uwekezaji lililofanyika visiwani Zanzibar na kuandaliwa na Equity Bank Tanzania, washiriki kutoka zaidi ya nchi 20 walijumuika kujadili fursa za kiuchumi zinazotokana na rasilimali za bahari. Tukio hili limekuja wakati ambapo serikali ya Zanzibar inalenga kufungua milango ya uwekezaji kupitia sera mpya na mazingira rafiki ya biashara.
Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda wa Zanzibar, Mhe. Omary Said Shaban, alisisitiza dhamira ya serikali kuboresha sheria, sera na miundombinu ili kuvutia wawekezaji. Alisema serikali iko tayari kushughulikia changamoto zote zinazoweza kukwamisha maendeleo ya uwekezaji, ili kuhakikisha wawekezaji wanafanya kazi katika mazingira bora.
“Tunataka mazingira yawe rafiki kwa mwekezaji na kwa taifa. Tupo tayari kushughulikia changamoto za kisheria, kiutendaji na miundombinu ili kuhakikisha wawekezaji wanapata kila hitaji muhimu la kuendesha shughuli zao kwa ufanisi,” alisema Waziri Shaban.
Akizungumza katika jukwaa hilo, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Rashid Ali Salim, alisema uchumi wa buluu ndio nyenzo kuu ya maendeleo ya Zanzibar, akitaja sekta kama uvuvi, utalii wa baharini, usafiri wa majini na miundombinu ya bandari kama maeneo yenye fursa kubwa za uwekezaji.
Aliishauri Equity Bank kuanzisha huduma za kifedha zinazozingatia misingi ya mabenki ya Kiislamu, kwa lengo la kuongeza ushirikishwaji wa wananchi katika huduma za kifedha na kusaidia jamii kunufaika moja kwa moja na fursa za uchumi wa buluu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Biashara wa Equity Bank Tanzania, Prosper Nambaya, alisema benki hiyo imejipanga kuwa mwezeshaji mkuu wa sekta binafsi kwa njia ya mitaji, ushauri wa kiufundi na mikutano ya kibiashara. Alisisitiza kuwa Equity inalenga kuhakikisha fursa hizi zinawanufaisha wanawake, vijana na biashara changa kupitia taasisi yake ya Equity Group Foundation.
Miongoni mwa washiriki wa kimataifa, Kavsel Kocadag, mwekezaji kutoka nje ya nchi, alieleza kuwa Zanzibar inaonesha mwelekeo mzuri wa kiuchumi unaovutia uwekezaji wa kimataifa. “Mikutano kama hii ni njia bora ya kutangaza vivutio na fursa za kiuwekezaji. Zanzibar inajitokeza kama eneo lenye matarajio makubwa ya kiuchumi barani Afrika,” alisema.