MKUFUNZI kutoka Chuo cha IIT Madras Bombay, Profesa Kannan M. Moudgalya, amewataka washiriki wa mafunzo ya programu ya Spoken Tutorials kuitumia ipasavyo fursa hiyo adhimu, akieleza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ujuzi wa TEHAMA, hasa katika mazingira ya sasa ambapo teknolojia imeshika nafasi kubwa katika sekta mbalimbali nchini.
Akizungumza katika mafunzo ya siku tatu yaliyowahusisha walimu, wanafunzi wa vyuo vikuu pamoja na wanafunzi wa kidato cha tano na sita, yaliyofanyika katika Kampasi ya Zanzibar ya IIT Madras iliyopo Bweleo, Wilaya ya Magharibi B Unguja, Prof. Kannan alisema programu hiyo ni nyenzo muhimu inayowasaidia wanafunzi kuelewa masuala ya TEHAMA kwa haraka na kwa njia rahisi.
Alifafanua kuwa Spoken Tutorials ni jukwaa linalotoa mafunzo kwa njia ya video zinazojieleza hatua kwa hatua, hivyo kumwezesha mwanafunzi kujifunza bila uhitaji wa mwalimu wa moja kwa moja. Hili linaongeza nafasi ya mwanafunzi kuelewa kwa undani zaidi kupitia kujifunza kwa vitendo.
Aidha, Prof. Kannan alisema kuwa mpango wa kutafsiri video hizo kwa sauti (dubbing) ulianza zaidi ya miaka 15 iliyopita nchini India, kwa lengo la kuwafikia wanafunzi wa maeneo ya pembezoni waliokuwa wakikosa walimu bora na waliokuwa hawawezi kumudu gharama za programu za kompyuta.
Alisema kuwa kupitia mpango huo, maelfu ya wanafunzi nchini India wameweza kuongeza ujuzi wao wa TEHAMA na wengi wao wamefanikiwa kuajiriwa au kujiajiri katika sekta ya teknolojia. Alieleza kuwa mafanikio kama hayo yanawezekana pia Zanzibar endapo vijana wataitumia ipasavyo fursa waliyoipata.
Prof. Kannan alihimiza washiriki waendelee kutumia majukwaa ya kujifunza kwa njia ya mtandao na wasisite kuwashirikisha wenzao ili kuwasaidia pia kunufaika na fursa hiyo. Alisema teknolojia ikitumika ipasavyo, inaweza kuleta mapinduzi makubwa katika mfumo wa elimu.
Alihitimisha kwa kusema kuwa malengo makuu ya Spoken Tutorials ni kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujifunza kwa uhuru, kuwa wabunifu na kuhimili ushindani wa soko la ajira la kidijitali, ambalo linazidi kuhitaji watu wenye maarifa ya teknolojia ya kisasa.
Washiriki wa mafunzo hayo walionesha shukrani kwa kuhusishwa katika programu hiyo. Kauthar Omari kutoka Skuli ya Biashara alisema mafunzo hayo yamempa mwanga mpya kuhusu matumizi ya kompyuta, kwani njia ya mafunzo kwa video ni rahisi kueleweka kuliko maelezo ya darasani pekee.
Naye Maryam Hassan Vuai kutoka Zanzibar Commercial Secondary School alisema programu hiyo itamuwezesha kuelewa kwa kina somo la TEHAMA na kuongeza uwezo wake wa kufaulu mitihani, pamoja na kumwandaa kutumia teknolojia katika maisha ya kila siku na baadaye katika ajira.
Wanafunzi hao walieleza kuwa mara nyingi katika mazingira ya skuli, muda na vifaa vya kujifunzia TEHAMA ni haba, lakini kupitia Spoken Tutorials wanaweza kujifunza kwa wakati wao binafsi hata nje ya darasa, jambo litakalowasaidia kujijengea uwezo wa kujitegemea katika kujifunza.