Na Mwandishi Wetu, Arusha
Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Korea (KOICA), kimezindua rasmi maabara ya kisasa ya 3D Design yenye lengo la kuwajengea wanafunzi wa Kitanzania ujuzi wa kisasa katika fani za uhandisi na ubunifu.
Uzinduzi huo umefanyika Mei 23, mwaka huu, na umeashiria kukamilika kwa mradi unaojulikana kama “Uanzishwaji wa Maabara ya 3D Design na Uimarishaji wa Uwezo wa Ubunifu katika Uhandisi wa Mitambo”.
Mradi huo umegharimu jumla ya Dola za Marekani 24,000, ambapo KOICA ilichangia Dola 20,000 na ATC Dola 4,000. Maabara hiyo ina vifaa vya kisasa vikiwamo kompyuta zenye uwezo mkubwa, mashine za kuchapisha vitu kwa teknolojia ya 3D (3D printers), skrini kubwa pamoja na programu maalum kama AutoCAD na SolidWorks.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi wa KOICA nchini Tanzania, Manshik Shin, alisema uwepo wa maabara hiyo ni hatua kubwa katika kuinua ubora wa elimu ya ufundi nchini.
“Teknolojia ya 3D siyo tu kifaa bali ni ujuzi muhimu kwa zama hizi za kidigitali. Hii ni fursa kwa vijana wetu kuwa na ushindani katika soko la ajira,” alisema.
Shin aliongeza kuwa mradi huo unalenga kusaidia kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan Lengo la 4 (Elimu Bora), Lengo la 8 (Ajira na Ukuaji wa Uchumi) na Lengo la 10 (Kupunguza Ukatili wa Kijinsia), hasa kwa kuwajengea uwezo wanafunzi wa kike.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha, Profesa Musa Chacha, aliishukuru KOICA kwa mchango wake mkubwa na kueleza kuwa maabara hiyo itatumiwa na wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali nchini.
“Maabara hii ni kwa ajili ya Watanzania wote wanaotaka kuongeza maarifa ya uhandisi wa kisasa. Hili ni jukwaa la pamoja la maarifa, utafiti na uvumbuzi,” alisema Profesa Chacha.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi, Elisha B. Mwakitaja kutoka Idara ya Mechatronics na Materials Engineering alisema msaada huo umeongeza chachu ya kujifunza na kuwaandaa wanafunzi kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia duniani.
Maabara hiyo inatarajiwa kunufaisha zaidi ya wanafunzi 430, wakiwemo idadi inayoongezeka ya wanafunzi wa kike, na kuiweka ATC katika ramani kama kituo bora cha kitaifa kwa elimu ya vitendo ya uhandisi na ubunifu wa muundo