
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, ambaye pia ni Mkurugenzi wa kampuni ya ARUL PRODUCT, Bi. Khalima Chembamoyo, ameibuka mshindi wa Tuzo ya Mjasiriamali Bora katika hafla ya utoaji wa Tuzo za Malkia wa Dhahabu zilizofanyika mkoani Geita.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Bi. Chembamoyo alisema kuwa tuzo hizo ni njia nzuri ya kutambua na kuthamini mchango wa wanawake katika jamii, hususan katika sekta ya ujasiriamali. “Tuzo hizi zinaongeza hamasa na mwitikio chanya kwa wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na kujitambua kama nguzo muhimu ya jamii,” alisema Chembamoyo.
Tuzo za Malkia wa Dhahabu hutolewa kwa lengo la kuwahamasisha wanawake na kuwapa motisha ya kuendelea kuchangia katika ustawi wa jamii kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.