Na Said Mwishehe,Michuzi TV
Ni mwendo wa nyamachoma tu! Hivi ndivyo unavyoweza kuelezea yanayoendelea katika soko la nyama choma la Kumbilamoto lililopo Vingunguti jijini Dar es Salaam.
Soko la nyama choma la Kumbilamoto lilizinduliwa Mei 24 mwaka huu na Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa na kushuhuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Mkoa na Halmashauri ya Wilaya ya Ilala.
Katika uzinduzi huo mwenyeji wao alikuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam Omari Kumbilamoto ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Vingunguti.Ujenzi wa soko hilo umegharimu shilingi zaidi ya milioni 700.
Tangu kuzinduliwa kwa soko hilo mamia ya wakazi wa Dar es Salaam na hasa ambao wanaishi maeneo ya karibu na soko hilo sasa wanajinoma tu na nyama choma.Utawaambia nini? Ni mwendo wa nyama choma tu.
Halafu soko lenyewe limekaa karibu na machinjio ya nyama Vingunguti.Lilipo soko na machinjio ya nyama wametanganishwa na barabara tu.Watu wanafaidi.Wajasiriamali wanainjoi laifu.
Kuna wakati unaweza kusema mbona soko hili limechelewa lakini kwa tunaoamini kila jambo na wakati wake ,tunasema wakati ndio huu.Watu wa Dar es Salaam hakuna sababu ya kuwaza kuhusu wapi utapata nyama choma tena tamu na laini.
Njoo vingunguti ,uliza soko la nyama choma liko wapi? Unaelekezwa tena kiroho safi kabisa.Wale wapenzi wa nyama choma tukutane soko la nyama Kumbilamoto.Ukitaka na ugali unapata,Mama Lishe na baba lishe nao wameamua kupiga kambi…
Katika soko hili nikiri kuna wachoma nyama wengi kuna mshikaji anaitwa Shaban nyama hatari,sio kwamba nampigia debe ila jamaa kwa kweli anajua kuchoma nyama,watu kibao.Kuna vimchuzi fulani hivi halafu vimewekwa na ndimu.Huyu Shaban Nyama anajua bwana.Acha tuachane na Shaban Nyama.Usije sema namfagilia bure.Ukifika utaamua unachoma nyama kwa nani.
Hata hivyo katika eneo hili ninachoweza kusema Meya wa Jiji la Dar es Salaam Kumbilamoto kuna namna ameweza kuifanya katika kuinua maisha ya wajasiriamali hapa Vingunguti,watu wanapiga pesa tu, unafanya masihara na nyama choma.Kwa wale ambao wanafahamu mnadani Dodoma watakuwa wananielewa.
Leo Mei 31,2025 nimekuja kula nyama choma halafu Meya Kumbilamoto alivyokuwa na ubunifu utakutana na burudani za muziki mkali,inategemea DJ ameamua aweke nyimbo gani? Kwa mimi mpenzi wa Singeli zinapigwa za kutosha.
Nimekuja hapa nimesahau kama kuna kufa,mawazo ya kufa yanatoka wapi wakati roho inapata kitu inapenda,Natamani maeneo ya nyama choma yawe mengi katika Jiji la Dar es Salaam.Wananchi wawe wanaamua wanataka kwenda kula nyama choma wapi.
Hata hivyo kwa sasa ni hapa soko la kumbilamoto vingunguti.Halafu hakuna kulala.Saa sita usiku ni kama mchana ,watu wa Dar si unawajua tena kwa mtoko.Wenye familia ruksa kwani usalama upo wa kutosha .Hata hivyo kujilinda mwenyewe ruksa.Si unajua tena kwenye wengi kuna mengi.
Kabla sijahitimisha naomba nitoe pongezi kwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira tulivu ya nchi yetu kiasi kuwezesha wananchi kufanya shughuli zao wakiwa salama salmini,lakini nampongeza Rais Samia kwa kutoa fedha kufanikisha soko hilo.Limejengwa kisasa sana.
Salamu pia ziende kwa Meya ya Jiji la Dar es Salaam Omar Kumbilamoto kwa kuhakikisha ujenzi wa soko hilo unafanyika,unakamilika na sasa watu wanakula nyama choma.Ubunifu uliofanyika katika soko hilo ni mkubwa sana.Lakini pongezi kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala na Mkurugenzi wa Ilala kwa kusimamia vema ujenzi wa soko la Kumbilamoto.
Kwa wakazi wa Vingunguti nadhani kwa sasa wamepata eneo ambalo limewaongezea fursa ya kufanya biashara saa 24.Kinachofurahisha zaidi wanaofanyabiashara ni wananchi wa kawaida kabisa.
Hata ukiwa na buku unapata nyama kisha ugali utaelewana na mama Lishe.Inategemea tu nguvu ya tumbo lako.Njoo bwana kwa Kumbilamoto mbona fresh tu.Inatosha kwa leo acha niendelee kula kidari cha mbuzi.
Pamoja na hayo naomba niseme kwa msisitizo kwamba katika soko hilo leo Mei 31 kunafanyika Tamasha la kumpongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha wajasiriamali .Hakika tamasha la kumpongeza Rais Samia hapa soko la nyama choma limeandaliwa kwa kiwango kikubwa.Halafu Benki ya CRDB wamelinogesha vema tamasha hili.
Narudia tena na hapa unielewe ni hivi Rais Samia amekuwa mstari mbele katika kuboresha maisha ya wananchi kwa kuweka mazingira mazuri ya kufanya shughuli za utafutaji.Ukifika katika Soko la Vingunguti utanielewa ninachokueleza .Hongera Rais Samia na kwa kuwa huu ni wa Uchaguzi Mkuu basi niseme tu Watanzania wenzangu hasa wa Dar es Salaam na Vingunguti MITANO TENA KWA DK.SAMIA.