Na Mwandishi Wetu
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limewajengea uwezo wajasiriamali zaidi ya 700 kutoka Manispaa ya Ubungo kuhusu namna ya kuchangamkia fursa ya kuwekeza katika nishati mbadala ya Rafiki Briquettes, ambayo ni rafiki kwa mazingira na nafuu kwa matumizi ya kila Mtanzania.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo wakati akifungua semina hiyo, iliyofanyika leo, Mei 30, 2025, jijini Dar es Salaam, Afisa Mazingira wa Manispaa hiyo, Bi. Jesca Stanley, amesisitiza umuhimu wa kutumia nishati mbadala si tu kwa ajili ya kulinda mazingira, bali kama fursa ya kiuchumi kwa vijana na jamii kwa ujumla.
Bi. Stanley amesema kuwa Manispaa ya Ubungo itaendelea kutengeneza mazingira rafiki pamoja na kuwawezesha vijana kwa kuwajengea uwezo katika matumizi ya nishati mbadala, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu na uhifadhi wa mazingira Kitaifa.
“Watu wenye sifa wafike katika Ofisi ya Maendeleo ya jamii Manispaa ya Ubungo kwa ajili ya kupewa utaratibu wa kupata mikopo na baada ya kupata tunaomba watumie kulingana na vigezo walivyopewa kupata mikopo jambo ambalo litasaidia kufanya marejesho” amesema Stanley.
Kwa upande wao, Afisa Masoko Mwandamizi wa STAMICO, Bw. Bilton Otto, pamoja na Afisa Masoko, Bw. Mark Stephano, wameeleza kuwa kuna fursa kubwa ya biashara katika nishati mbadala ya Rafiki Briquettes kutokana na gharama yake kuwa nafuu na manufaa ya kimazingira.
“Tumefadhili wajasiriamali zaidi ya 700 ili waweze kupata mafunzo katika semina hii, mwitikio ni mkubwa na wengi wameonesha nia ya kuwa mawakala wa bidhaa ya nishati mbadala ya Rafiki Briquettes baada ya kuona umuhimu na faida katika matumizi ukilinganisha na nishati nyengine” amesema Bw. Bilton Otto.
Bw. Stephano amesema kuwa STAMICO imekuja na bidhaa hiyo kwa lengo la kuwasaidia watanzania kuondokana na ukosefu wa nishati ya kupikia, hivyo ni wakati wa vijana kuanzishaji vikundi kwa ajili ya kupata mkopo kwa kushirikiana na Manispaa ya Ubungo kwani uhitaji ni mkubwa.
Amebainisha kuwa kwa mujibu wa takwimu mbalimbali, Mkoa wa Dar es Salaam ni miongoni mwa mikoa yenye matumizi makubwa ya mkaa, ambapo takribani tani milioni moja hutumika kwa mwaka.
“STAMICO tumekuja na bidhaa hii kwa lengo la kuonesha fursa zilizopo, tukishirikiana na Manispaa ya Ubungo ili kuwawezesha wajasiriamali kupitia mikopo rasmi na kuhamasisha vijana kuwa mawakala wa nishati mbadala ya Rafiki Briquettes,” amesema
Nao baadhi ya wajasiriamali wa Manispaa ya Ubungo walioshiriki semina hiyo, akiwemo Asinath Jameson na Julius Msele, wamelishukuru Shirika la STAMICO kwa kudhamini mafunzo kwani yamekuwa na msaada mkubwa kwao pamoja na kupatiwa fursa ya kipekee ya kuingia katika biashara ya nishati mbadala ya Rafiki Briquettes