Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Watendaji Wizara Wizara ya Kilimo watakiwa kuanza mchakato wa ununuzi wa ndege mpya tatu kwa ajili ya vituo vya Kilimo anga vya kanda vilivyopo katika mikoa ya Arusha,Mbeya na Mwanza lengo likiwa ni kudhibiti visumbufu vya mimea.
Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe, ametoa maagizo hayo wakati wa hafla ya mapokezi ya ndege moja ya kudhibiti visumbufu vya mimea iliyonunuliwa na Serikali chini ya Wizara hiyo kwenye Kiwanja kidogo cha ndege Mkoani Dodoma ambayo itatumika katika kituo cha Kanda ya Kati.
“Vituo vyote hivi vinatakiwa viwe vina ndege na ‘drones’ kwa hiyo, mchakato wa kununua ndege tatu nyingine uanze sasa hivi. Ni lazima kama Nchi ijitegemee, dunia ya kubebana haipo. Lazima tuweze kutoa huduma, tumeshaanza kununua ‘drones’ za kufanya ‘survilence’, mwaka huu tunanunua drone kwa ajili ya ‘spraying’.” Mhe. Bashe.
Kadhalika, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) Prof. Joseph Ndunguru, amesema ndege hiyo inalenga kuleta mageuzi makubwa katika Sekta ya Kilimo kwa kuleta tija, ajira na kupanua masoko lakini pia kuimarisha hali ya chakula hapa nchini na kuongeza kuwa visumbufu vya mimea ni moja ya jitihada za Mamlaka katika kuleta tija kwenye sekta hiyo.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule ameishukuru Wizara ya Kilimo kwa ununuzi wa Ndege hiyo ambayo italeta matumaini kwa Mkulima.
“Utashi huu unakwenda kuleta matumaini kwa Mkulima ambaye si mvivu, kwani amelima na kutunza mazao yake halafu mwishoni ndege anakula. Kwa Mkoa wa Dodoma itatuongezea upatikanaji wa chakula na wale wavivu sasa wataanza kulima kwani Dodoma pia tunapata athari ya Nzige maeneo ya Bahi na Kwelea kwelea maeneo ya Chemba, Kondoa na Kongwa.”