Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Serikali ya China katika nyanja mbalimbali, ikiwemo timu ya madaktari kutoka China wanaokuja kutoa huduma za kibingwa katika hospitali za umma, pamoja na fursa za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Zanzibar.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipokutana na Balozi Mdogo mpya wa China, Mhe. Li Quanghua, aliyefika Ikulu Zanzibar leo 02 Juni 2025, kwa ajili ya kujitambulisha rasmi pamoja na ujumbe wake.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi ametaja maeneo mahususi ya ushirikiano ambayo Serikali ya Zanzibar imeyapa kipaumbele, yakiwemo: kuhamasisha uwekezaji kutoka China, kukuza biashara baina ya pande mbili, na kuimarisha programu za kuwawezesha vijana kupitia mafunzo ya ufundi stadi ili kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana wengi wanaokosa ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano katika sekta ya utalii, hususan kwa kuangazia uwezekano wa kuanzishwa kwa safari za moja kwa moja za ndege kati ya China na Zanzibar hatua itakayosaidia kuongeza idadi ya watalii, kukuza mahusiano ya kitamaduni, na kuimarisha uchumi.
Kwa upande wake, Balozi Li amemshukuru Rais Dkt. Mwinyi kwa ukarimu mkubwa alioupokea tangu alipowasili, na kueleza kuwa katika kipindi kifupi alichokuwepo Zanzibar, ameweza kutembelea miradi mbalimbali na kuridhishwa na kasi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Rais Dkt. Mwinyi.