Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amepiga marufuku kwa Halmashauri mkoani humo kuendelea kukopa au kulimbikiza madeni kwa watoa huduma wa ndani, akieleza kuwa kitendo hicho kinazorotesha mitaji na kudumaza maendeleo ya uchumi wao.
Kanali Mtambi alitoa agizo hilo wakati wa kikao cha kujadili utekelezaji wa mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kilichofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, mkoani Mara.
Amesema ni muhimu kwa Halmashauri kuhakikisha wanatenga sehemu ya mapato yao ili kuwalipa kwa wakati watoa huduma, badala ya kushikilia fedha zao kwa miaka mingi na kuathiri ukuaji wa biashara zao.
“Madiwani hakikisheni mnasimamia mipango na bajeti zenu. Miongoni mwa vipaumbele vya Halmashauri ni kuhakikisha makusanyo ya mapato yanalenga kuwalipa watoa huduma wetu, hususan wa ndani. Ukimkuza mtoa huduma wa ndani, unakuza uchumi wa Halmashauri. Lakini ukimporomosha, unajiua mwenyewe,” alisema Kanali Mtambi.
Aidha, aliwataka viongozi wa Halmashauri kuhakikisha kila fedha inayokusanywa inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kwa uwazi ili kujenga imani kwa wananchi na wadau wa maendeleo.