Na Mwandishi wetu Dodoma.
Kikao kazi cha kupitia na kuthibitisha Rasimu ya Mpango Mkakati wa Taifa wa Kuzuia Kuzama Maji chafanyika tarehe 11 Juni, 2025 katika ukumbi wa Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto na uokoa Jijini Dodoma.
Kikao hicho kimewashirikisha Wawakilishi kutoka Wizara, Taasisi na Idara za Serikali, Mashirika ya Kimataifa, Asasi zisizo za Kiserikali, Mikoa mbalimbali ikiwemo Mwanza na Mara.
![]() |
Akifungua kikao hicho, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Kanali Selestine Masalamado amesema Nchi yetu imeendelea kukumbwa na matukio mbalimbali ya majanga ya asili na yanayosababishwa na shughuli za kibinadamu, ambayo yamekuwa na madhara makubwa kwa maisha ya wananchi hasa waishio pembezoni mwa fukwe wakiwemo Wazee, Vijana na Watoto, hivyo kuathiri maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Hata hivyo Kanali Masalamado amesema, Kutokana na majanga hayo, Serikali ilianza Mchakato wa kuandaa mkakati wa Taifa wa Kuzuia Kuzama Maji mwaka 2024, kwa lengo la kuanzisha mfumo madhubuti na jumuishi wa kupunguza matukio ya vifo vinavyotokana na kuzama maji.
Ameongeza kwa kusema, Mkakati huu umeandaliwa kwa njia shirikishi, ukihusisha wadau kutoka sekta mbalimbali, ili kuhakikisha hatua zinazopendekezwa zinajengwa juu ya ushahidi wa kisayansi, uzoefu wa jamii, na muktadha halisi wa Tanzania.
Ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa washiriki wote kuchangia mawazo yao kwa weledi na uzalendo katika kupitia na kuboresha Rasimu ya Mkakati, ili ifikie viwango vinavyostahili kabla ya kuidhinishwa rasmi na kuanza kutekelezwa.
Mwisho