Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dk. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 16.06.2025 amezindua jengo la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Simiyu na kuwataka Watanzania kujenga utamaduni wa kulipa Kodi kwa hiari ili kuiwezesha Nchi kujitegemea kiuchumi.
Rais Samia amesema kujitegemea kiuchumi kunaletwa na Wananchi kupitia Kodi wanazolipa na kuitaka TRA kuendelea kukusanya Kodi kwa njia rafiki kwa wananchi na kuwapatia elimu ya Kodi wananchi ambao hawana uelewa wa masuala ya Kodi.
Amesema kutegemea msaada ni utumwa hivyo TRA kupitia Kodi zinazokusanywa zimekuwa zikitekeleza miradi ya kijamii kama vile kupeleka Maji, Umeme na Huduma za Afya nchi nzima na katika miradi mikubwa ndiyo nchi imekuwa ikikopa au kupata msaada wa kutekeleza.
“Tunataka TRA ikusanye zaidi ndiyo maana tumewaongezea nguvu Kazi na majengo ya kisasa, nendeni mkakusanye kodi kwa njia rafiki, lakini kwa wale masugu na viburi lazima nao wafanywe walipe Kodi kama ilivyo kwa wengine” amesema Rais Samia.
Aidha Rais Samia ameagiza kuongezwa kwa kasi ya ujenzi wa majengo ya TRA ambayo bado hayajakamilika ili yaanze kutoa huduma katika mazingira rafiki.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema jengo hilo limegharimu kiasi cha Sh. Bilioni 9.83 na ni miongoni mwa majengo mengine yanayojengwa nchi nzima kwa gharama ya Sh. Bilioni 116.
Kamishna Mkuu Mwenda amesema jengo hilo na mengine yanayoendelea kujengwa nchini yataongeza utoaji huduma bora kwa Mlipakodi, yataongeza hamasa kwa Watumishi pia yataongeza makusanyo ya Kodi kwa ujumla.
“Mhe. Rais tunashukuru kwa kutupatia fedha za ujenzi wa majengo yote yaliyokamilika na yanayoendelea kujengwa hii itasaidia tuendelee kukusanya Kodi na kuvuka malengo kama ilivyokuwa kwa miezi 11 mfululizo tangu kuanza mwaka wa fedha 2024/2025 pia tunashukuru umetuongezea nguvu Kazi ya Watumishi wapya 1896” Kamishna Mkuu Mwenda amesema.
Kamishna Mkuu Mwenda amesema katika kipindi cha miezi 11 TRA ilitakiwa kukusanya Sh. Trilioni 27.841 lakini imekusanya Sh. Trilioni 28.861 sawa na ufanisi wa asilimia 105 na anatarajia mwezi uliosalia wa June watavuka malengo.