Songea-Ruvuma.
Katika kuadhimisha wiki ya usalama wa miundombinu ya TANESCO, Afisa Usalama Mkuu Msaidizi kutoka Kitengo cha Uzuiaji Makao Makuu ya TANESCO, Shami Yusuph Dunia, ametoa wito kwa wafanyakazi na jamii kushirikiana kwa karibu kuhakikisha ulinzi wa miundombinu ya shirika hilo.
Akizungumza na wafanyakazi wa TANESCO mkoani Ruvuma leo Juni 16, 2025, Dunia amesema kuwa jukumu la kulinda miundombinu ya shirika si la idara ya usalama peke yake, bali linamhusu kila mfanyakazi na mwananchi. Amefafanua kuwa kazi ya usalama ni pamoja na kuzuia na kuchunguza matukio ya uharibifu au wizi wa vifaa vya shirika, hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za umeme kwa ufanisi.
Ameeleza kuwa kwa kuwa TANESCO ni shirika lenye mtandao mpana wa kitaifa, ni vigumu kwa idara ya usalama pekee kukabiliana na vitendo vyote vya kihalifu, hivyo ni muhimu kila mfanyakazi kuhakikisha miundombinu kama njia za kusafirisha umeme, mabwawa, mita, magari ya shirika, na vifaa vingine inalindwa muda wote.
Dunia amesisitiza kuwa jamii nayo ina nafasi muhimu katika mapambano dhidi ya uharibifu wa miundombinu, hasa wakati huu ambapo vitendo vya uharibifu na wizi wa vifaa vya umeme vinaongezeka, ameitaka jamii kuwa walinzi wa mali za umma kwa kutoa taarifa pindi wanaposhuhudia au kupata taarifa za uhalifu.
Aidha, amewatahadharisha wafanyakazi kuhusu kuongezeka kwa matapeli wanaowalaghai wateja kwa kutumia jina la TANESCO, ametoa wito kwa wafanyakazi kuwa walinzi wa wateja kwa kuhakikisha hakuna mtu asiyehusika anayewafikia kabla ya maafisa halali wa shirika, huku akihimiza utoaji wa taarifa haraka kwa uongozi pale vitendo hivyo vinapogundulika.
Kwa upande wake, Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Ruvuma, Alan Njiro, amewakumbusha wafanyakazi ngazi ya jamii kutumia elimu waliyopatiwa kufikisha taarifa sahihi kwa wananchi, amesema watumishi hao ndio wanaokutana na wananchi mara kwa mara, hivyo wana nafasi ya kipekee katika kuwaelimisha kuhusu ulinzi wa miundombinu ya umeme.
Mafanikio ya TANESCO kama mtoa huduma wa umeme nchini yanategemea kwa kiwango kikubwa uimara na usalama wa miundombinu yake. Ushirikiano wa karibu kati ya wafanyakazi, wananchi na uongozi wa shirika ni silaha muhimu katika kuhakikisha miundombinu inalindwa dhidi ya uharibifu na wizi, Kwa pamoja kupitia uzalendo na uwajibikaji, TANESCO inaweza kuimarisha utoaji wa huduma bora na endelevu kwa Watanzania wote.