Na Diana Byera,Bukoba.
Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini ametoa msaada wa vifaa vya ujenzi wa jiko la wafungwa kwenye Gereza la Kilimo Rwamurumba vyenye thamani ya shilingi Milioni 1.3
Akizungumza wakati akikabidhi msaada huo Rweikiza amebainisha kuwa ameguswa na adha wanayopata wafungwa wakati wa kuandaa chakula chao kwenye jiko lililoharibika hasa nyakati za mvua .
Amesema kuwa taarifa ya ubovu wa jiko hilo aliipokea kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ambaye ni mkuu wa Wilaya ,Erasto Sima ndipo akachukua uamuzi wa kuwajibika kama kiongozi.
Alitoa wito kwa jamii kujitoa kwani Gereza ni sehemu inayotoa huduma za jamii kama kurekebisha makosa na kuendelea kurekebisha maadili hivyo wadau wa maendeleo wasijitenge na maeneo kama hayo.
Mkuu wa wilaya ya Bukoba Erasto Sima amemshukru mbunge huyo kwa kusikia kilio chao huku akiwaomba wananchi kuwakumbuka wafungwa licha ya kuwa serikali ndiyo yenye jukumu la kuwatunza.
“Serikali inashughulikia miradi Mingi,nimefurahishwa na Mbunge huyu alivyosikia kilio hiki kutoka kwangu kama kiongozi ameunga mkono haraka kwa sababu wafungwa walioko Hapa wanatoka kwenye jamii yetu ,wanapaswa kuishi katika mazingira mazuri na wadau tunapaswa kuelewa Hilo”Amesema Sima
Hata hivyo Mkuu wa Gereza hilo Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Magereza Benard Baroga amekiri kupokea vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi milioni moja na laki tatu (1,300,000/=)huku akimshukru kwa kijitoa kwake katika kuboresha jiko la wafungwa.