
Kikosi cha wanawake kutoka kwenye miamba ya dhahabu, mkoani Geita , Geita Queens kimefanikiwa kurejea tena katika Ligi Kuu ya Soka la Wanawake Tanzania kwa mara ya pili, kufuatia ushindi muhimu walioupata jijini Mwanza.
Mara baada ya kurejea mkoani Geita, timu hiyo ilipokelewa kwa shangwe na viongozi wa Chama cha Soka Mkoa wa Geita (GEREFA) pamoja na viongozi wa Chama cha Soka la Wanawake mkoani humo.
Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Mwenyekiti wa Soka la Wanawake mkoa wa Geita, Elizabeth Makwenda, alisema kuwa mafanikio hayo ni faraja kubwa kwao na jamii kwa ujumla. Alitoa wito kwa wadau na mashabiki wa soka kuendelea kuiunga mkono Geita Queens ili iendelee kufanya vizuri.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Geita, Salum Ally Kulunge, alisema kuwa wamejifunza kutoka makosa ya nyuma yaliyosababisha kushuka daraja, na kwa sasa wamejipanga kuhakikisha hali hiyo haijirudii. Alitumia fursa hiyo kuwashukuru wadhamini wakuu wa timu hiyo, African Underground, kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha mafanikio haya.
Kocha Mkuu wa Geita Queens, Ally Kitula, alisema siri ya mafanikio yao ni nidhamu, kujituma na mshikamano miongoni mwa wachezaji. Aliahidi kuwa wataendelea kupambana ili kuhakikisha timu inabaki katika ligi kuu kwa msimu ujao.
Naye Nahodha wa timu hiyo, Honesta Hamidu, alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wadau wote waliojitokeza kuwaunga mkono katika safari yao ya kurejea ligi kuu, huku akiahidi kutowavunjia moyo mashabiki wao.