Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali nchini, Bavoo Junus, amesema kuwa Kongamano la Kitaifa la Sheria litafanyika kesho Jumamosi, Juni 21, 2025, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali amesema hayo leo Juni 20, 2025, jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari, ambapo amesema kuwa mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete, na kongamano hili linaandaliwa na Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania.
“Moja kati ya malengo ya kuanzishwa kwa Chama cha Mawakili wa Serikali ni kuwaunganisha mawakili wa serikali wanaotoka katika maeneo mbalimbali, kuwaleta pamoja ili kuweza kujadili masuala mbalimbali yanayohusu sheria, lakini pia lengo lingine la msingi la kuanzishwa kwa chama ni kukifanya chama kiwe jukwaa la kutoa elimu na mafunzo kwa wananchi kwa sababu serikali inawajibika kwa wananchi, kwa maana hiyo sisi ni mawakili wa wananchi,” amesema Junus.
Aidha, ameongeza kuwa Chama cha Mawakili kina jukumu la kutoa elimu katika masuala mbalimbali ya kisheria, hususan katika mambo yanayogusa maslahi mapana ya taifa. Sasa katika kutekeleza jukumu la kutoa elimu kwa umma, na kwa kuzingatia tunaenda katika uchaguzi mkuu, chama kimeandaa kongamano ambalo lengo lake kubwa ni kutoa elimu kwa wananchi kuhusu sheria mbalimbali zinazohusu uchaguzi mkuu.