TBS Yazindua Rasmi Tuzo za Ubora Kitaifa – Awamu ya Sita
-Washindi wa kitaifa kupata nafasi ya kushiriki maonyesho ya SADC nchini Madagascar
Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limezindua rasmi mashindano ya Tuzo za Kitaifa za Ubora kwa msimu wa sita ambayo ni mahususi katika kuhamasisha utamaduni wa kuthamini ubora wa bidhaa na huduma nchini.
Pia tuzo hizo zinalengo la kutoa motisha kwa taasisi na watu binafsi wanaozingatia viwango katika uzalishaji na utoaji huduma.
Akizungumza na waandishi wa habari Juni 20, 2025 Jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, amesema kuwa mashindano hayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuimarisha ushindani wa bidhaa na huduma za Tanzania kwenye soko la kimataifa.
“Tumeamua kuwekeza zaidi katika ubora kwa kuwa hii ndiyo njia pekee ya kuhakikisha bidhaa na huduma za Tanzania zinaweza kushindana kimataifa, hasa katika zama hizi za biashara huria,” alisema Dkt. Katunzi.
Mashindano ya mwaka huu yatajumuisha vipengele saba vikuu, ikiwemo Kampuni bora ya mwaka, Bidhaa bora ya mwaka, Huduma bora kutoka taasisi binafsi na za umma, pamoja na tuzo kwa wauzaji bora wa bidhaa nje ya nchi na mchango wa mtu binafsi katika ubora.
Kipengele cha kwanza hadi cha sita kitakuwa na makundi mawili: kwa kampuni kubwa na kwa wajasiriamali wadogo.
Kwa mujibu wa TBS, lengo la mashindano haya ni kuhamasisha utamaduni wa kuthamini ubora wa bidhaa na huduma nchini, sambamba na kutoa motisha kwa taasisi na watu binafsi wanaozingatia viwango katika uzalishaji na utoaji huduma.
Aidha, Dkt. Katunzi alisema kuwa washindi wa tuzo hizo watawakilisha Tanzania katika mashindano ya ubora ya kikanda yanayoratibiwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Amesema katika mashindano ya mwaka uliopita, Tanzania ilifanikiwa kunyakua tuzo mbalimbali ikiwemo Kampuni bora ya mwaka kupitia Said Salim Bakhresa and Company Ltd, Bidhaa bora ya mwaka kupitia Kilombero Sugar Company Ltd, pamoja na Huduma bora ya mwaka ya mjasiriamali kupitia CAPS Tanzania Ltd.
Pamoja na hayo amesema kwa mwaka huu, washindi wa kitaifa watapata nafasi ya kushiriki katika Wiki ya Viwanda ya SADC itakayofanyika nchini Madagascar kuanzia tarehe 28 Julai hadi 2 Agosti 2025, fursa itakayowapa jukwaa la kutangaza bidhaa na huduma zao kwa nchi wanachama 16 wa SADC.
Hata hivyo amesema kuwa Maandalizi na tathmini ya mashindano hayo yanafanywa na Kamati Maalum inayojumuisha taasisi kama TBS, ZBS, TPSF, TCCIA, SIDO, TWCC, ZEEA, TANTRADE na NQAT.
Vidokezo vya ushiriki vinapatikana kupitia tovuti za TBS, ZBS na TPSF.
Mashindano haya yamefanyika kwa mafanikio tangu mwaka 2019, na kwa mara ya kwanza mwaka huu yameongeza vipengele kutoka vitano hadi saba ili kuleta usawa na kushirikisha taasisi nyingi zaidi.