NA BELINDA JOSEPH, SONGEA.
Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Ruvuma umewahakikishia wananchi 851 waliopisha mradi wa ujenzi wa barabara ya Likuyufusi-Mkenda kuwa watalipwa fidia mapema bila kuathiri shughuli zao za kiuchumi na kijamii. Fidia hiyo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 5 inatarajiwa kulipwa mara baada ya TANROADS kupokea fedha kutoka Wizara ya Fedha.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Fedinand Mdoe, wakati wa hafla ya kukabidhi rasmi awamu ya kwanza ya ujenzi wa barabara hiyo Likuyufusi–Mkayukayu yenye urefu wa km 60 kwa mkandarasi kutoka kampuni ya China First Highway Engineering Co. Ltd, iliyofanyika katika kijiji cha Litapwasi, Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Mhandisi Mdoe amesema uthamini wa mali za wananchi waliopisha mradi huo umefanyika na sasa mkandarasi yupo katika maandalizi ya kuanza utekelezaji wa mradi, ameongeza kuwa TANROADS itaweka utaratibu mzuri wa ulipaji wa fidia ikiwa ni pamoja na kuunda kamati za kushughulikia malalamiko yoyote yatakayojitokeza.
Mradi wa ujenzi awamu ya kwanza ya barabara ya Likuyufusi–Mkayukayu yenye urefu wa kilomita 60 unagharimu Shilingi Bilioni 110.77 na unatekelezwa kwa ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ujenzi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 27, ikijumuisha miezi mitatu ya maandalizi, ambapo mkataba wa utekelezaji ulisainiwa tarehe 10 Juni 2025.
Amesema Serikali pia imepanga kuanza utekelezaji wa awamu nyingine ya mradi huo, kutoka Mkayukayu hadi Mkenda (km 64) mara baada ya awamu ya kwanza kukamilika, pamoja na ujenzi wa madaraja ya Mitomoni na Mkenda, Mradi huo utaiunganisha Wilaya ya Songea na Nyasa, na pia utafungua lango muhimu la usafiri kati ya Tanzania na nchi jirani ya Msumbiji.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Songea, Kapenjama Ndile, alisisitiza umuhimu wa kuwapa wananchi taarifa sahihi kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao. Alisema ujenzi wa barabara hiyo utaongeza kasi ya maendeleo, uwekezaji, na kuimarisha shughuli za kiuchumi kutokana na ongezeko la wageni kutoka na kwenda Msumbiji.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Peramiho na Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, alieleza kuwa barabara hiyo itaimarisha usalama wa mipaka, kurahisisha shughuli za uzalishaji na kuunganisha wananchi na masoko ya ndani na nje ya nchi. Alitoa wito kwa wananchi kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara na shughuli za kilimo, mifugo na ujasiriamali ili kunufaika na fursa zitakazotokana na mradi huo.
Wakazi wa Kijiji cha Litapwasi, akiwemo Bali Tindwa na Felista Luena, walieleza furaha yao kuona hatua ya mradi kuanza rasmi kwa kukabidhiwa kwa mkandarasi. Walisema matarajio yao ni kuona mradi huo unakamilika kwa wakati ili kuwaondolea adha ya vumbi na matope, pamoja na kupunguza gharama za usafiri.
Walisema pia kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutachochea usafiri wa daladala, kuboresha shughuli za biashara, na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka vijijini kwenda mjini. Wameiomba serikali kumsimamia mkandarasi kwa karibu kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa ubora na kwa muda uliopangwa, na fidia kulipwa bila kuchelewa.