Mkuza Mitaala kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania Bw. Hemed Mdee amebainisha kuwa Taasisi ya Elimu Tanzania inaendelea na mafunzo maalumu kwa walimu wa somo la Biashara na Amali ili kuwasaidia kwenda kutekeleza Mtaala ulioboreshwa katika maeneo yao ya kazi.
Bw. Mdee amesema hayo leo Juni 23, 2025 katika mafunzo ya siku kumi ya kuwanoa walimu wa somo la Biashara na Amali yaliyofanyika katika chuo cha Ualimu Korogwe Jijini Tanga na kusisitiza mafunzo yanaendelea katika mikoa mingine ya Tabora na Morogoro.
“Nia na madhumuni ya mafunzo haya maalumu ni kuwanoa na kuwapa weledi wa kutosha walimu katika mbinu za ujifunzaji 8na ufundishaji ili wawe na umahiri wa kutosha katika namna ya kufikisha maudhui yanayotarajiwa kwa wanafunzi wetu.” Amesema Bw. Mdee
Aidha, amesisitiza kuwa, mafunzo haya ya siku kumi, yatamsaidia mwalimu kuwa na weledi wa kutosha wa kutumia mbinu mbalimbali za ufundishaji na ujifunzaji ili kuweza kufundisha kwa ufanisi.
Nae, Mnufaika wa mafunzo maalumu Mwl. Judith Mwalyego ambaye pia ni Mtaalamu wa masuala ya maji amesema mafunzo hayo yamekuja wakati mwafaka kwani yatawasaidia katika kuandaa masomo kwaajili ya kwenda kufundisha jambo litalosaidia katika utekelezaji wa Mtaala ulioboreshwa kwa ufanisi na tija.
Kwa upande wake Mwl. Halfani Mahamudu, Mtaalamu wa masuala ya maabara ambaye pia ni mnufaika wa mafunzo hayo maalumu ameishukuru Serikali kwa maboresho yaliyofanyika katika Mtaala, mbinu mbalimbali za kufundishia na kujifunzia, huku akisisitiza mbinu hizo wataenda kuzitumia katika maeneo yao ya kazi ili Mtaala huo ulete tija na mabadiliko chanya.