Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amewataka watumishi wa umma kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kuzingatia weledi, uadilifu na maadili ya utumishi wa umma.
Mhe. Majaliwa aliyasema hayo Juni 23, 2025, katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma, alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma.
Akizungumza mbele ya viongozi wa serikali, watumishi wa umma na wananchi waliojitokeza kushuhudia maadhimisho hayo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya kazi kwa watumishi wa umma, huku akiwasisitiza kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo kwa kutoa huduma zenye tija na huruma kwa wananchi.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema ni vyema kuimarisha mikakati ya kuhamasisha wananchi kujenga utamaduni wa kutumia fursa za uwepo wa maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma ili wajitokeze kwa wingi na kupata huduma zinazotolewa na Serikali kwa haraka zaidi.
Awali, wakati akizindua mfumo wa Kidijiti Mhe Majaliwa, alizitaka Taasisi zote za umma kutekeleza agizo la Mhe Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha kuwa Taasisi zenye mifumo na zinazoendelea kubuni mifumo inayosomana na zinazoweza kubadilishana taarifa kupitia mfumo huo ili kuboresha huduma ndani ya Serikali.
“Mamlaka ya Serikali Mtandao eGA hakikisheni kwamba mifumo iliyounganishwa inaendelea na majukumu yake ya kubadilishana taarifa lakini pia kila anayeingia mjiridhishe kuwa ana uwezo wa kuwasiliana na yeyote aliye kwenye mfumo’’. Alisema Mhe. Majaliwa.
Vile vile Mhe. Majaliwa aliwaasa watumishi wa umma kote nchini kujisajili katika mfumo wa kidijitali wa e – wezesha, ambao unawezesha watumishi wa umma kuwekeza moja kwa moja kupitia makato ya mshahara au mapato mbalimbali ya biashara.
Katika kuunga mkono maadhimisho hayo, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeungana na taasisi mbalimbali za umma kushiriki katika maonesho yanayofanyika kwa wiki nzima katika viwanja hivyo. Kupitia maonesho hayo TCAA inatoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake ya msingi, ikiwa ni pamoja na udhibiti wa shughuli zote za usafiri wa anga nchini.
Maeneo yaliyopewa kipaumbele na TCAA mwaka huu ni pamoja na usimamizi wa matumizi ya ndege zisizo na rubani (drones), ambao ni uwanja unaokua kwa kasi na unahitaji uangalizi wa karibu kwa ajili ya kulinda usalama wa anga, faragha ya wananchi na kuzuia matumizi mabaya ya vifaa hivyo katika maeneo yaliyokatazwa kama vile taasisi za serikali, kambi za kijeshi, na miundombinu nyeti.
Aidha, TCAA inatumia jukwaa hilo kutoa taarifa kuhusu huduma za uongozaji ndege, pamoja na kuhamasisha vijana na wadau kuchangamkia fursa za mafunzo zinazotolewa na Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania (CATC), ambacho kinamilikiwa na mamlaka hiyo.
Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu: “Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidijiti Ili Kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchagiza Uwajibikaji”, kaulimbiu inayolenga kuhimiza matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kuboresha huduma kwa wananchi na kuimarisha uwajibikaji wa watumishi wa umma.
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma huadhimishwa kila mwaka barani Afrika kuanzia Juni 16 hadi 23, yakihusisha taasisi mbalimbali za umma kuonesha huduma na mafanikio yao kwa wananchi kupitia maonesho ya wazi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Wiki ya Utumishi wa Umma kwenye Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma, Juni 23, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)