Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Shaban Ali Othman akikata utepe kuashiria uzinduzi wa ripoti ya Tathmini ya Mahitaji ya Teknolojia (TNA), uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaaam leo Juni 25, 2025 jijini Dar es Salaam.
.jpeg)
Viongozi mbalimbali wakionesha ripoti ya Tathmini ya Mahitaji ya Teknolojia (TNA), mara baada ya , uzinduzi uliofanyika jijini Dar es Salaaam leo Juni 25, 2025 jijini Dar es Salaam.
Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
SERIKALI imezindua rasmi ripoti ya Tathmini ya Mahitaji ya Teknolojia (TNA), hatua muhimu kuelekea mabadiliko ya kiuchumi yanayoendeshwa na sayansi, teknolojia na ubunifu.
Uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam leo Juni 25, 2025 na kuandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Teknolojia ya Umoja wa Mataifa kwa Nchi Zinazoendelea (LDCs), imeangazia teknolojia kama kichocheo kikuu cha maendeleo jumuishi na endelevu.
Akizungumza katika Uzinduzi wa ripoti hiyo Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Shaban Ali Othman amesema kuwa repoti hiyo ni katika kutambua mahitaji ya Teknolojia yaliyojikita katika maeneo mawili ya uvuvi pamoja na Kilimo.
Amesema kwa upande wa Zanzibar wanaeneo la kimkakati la ulimaji wa Mwani pamoja na ufugaji wa Samaki, ameeleza kuwa repoti hiyo itaenda kuwasaidia mahitaji mhimu katika uchumi wa buluu na kujua ni teknolojia ipi itahitajika na kwa kipindi gani ili ukulima wa Mwani, mbegu zinazotumika, Mahitaji ya soko pamoja na ufugaji wa mazao ya Samaki uwe na tija kwa wananchi.
Amesema kuwa Teknolojia za Usimamizi wa Takwimu, kama majukwaa ya kidijitali kwa kilimo na mifumo ya ufuatiliaji wa uvuvi itakuwa msaada mkubwa kwa jamii.
“Teknolojia hizi, licha ya kuhudumia sekta maalum, zinatajwa kuwa na matumizi mtambuka katika TEHAMA, elimu, viwanda, nishati, na madini zikihusishwa moja kwa moja na malengo ya taifa ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kuongeza usalama wa chakula, na kujenga mtaji wa watu wenye ujuzi wa kidijitali.”
Kwa upande wa Mwakilishi wa Muda wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Shigeki Komatsubara, amesisitiza kuwa ripoti hiyo ni zaidi ya nyaraka na ni dira ya kimkakati inayoweza kuleta mageuzi ya kweli katika sekta muhimu kama kilimo na uchumi wa buluu.
“Tanzania imepiga hatua muhimu katika safari yake ya maendeleo kwa kuzindua rasmi ripoti ya Tathmini ya Mahitaji ya Teknolojia (TNA) ambayo inalenga kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia teknolojia bunifu na mbinu za kisasa.”
Komatsubara aliwapongeza wadau mbalimbali waliohusika kuandaa TNA, akiwemo Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu, Mamlaka ya Bahari ya Kimataifa (ISA), Benki ya Teknolojia ya UN, sekta binafsi, taasisi za elimu ya juu na mashirika ya kiraia.
“Ripoti hii ni ushuhuda wa ushirikiano wa kweli,” amesema.
Amefafanua kuwa TNA inalingana kikamilifu na malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 huku pia ikichangia kwa kina katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Kwa mujibu wa hotuba hiyo, TNA imeweka bayana teknolojia zenye uwezo wa kubadilisha maisha ya Watanzania. Hizi ni pamoja na Kilimo kinachozingatia tabianchi (climate-smart agriculture),Mifumo ya data ya hali ya juu, Vifaa vya uchunguzi wa mbali (remote sensing tools), Miundombinu ya TEHAMA na mifumo ya fedha ya kidijitali, teknolojia za uvuvi wa kisasa (intelligent aquaculture)
Komatsubara ameeleza kuwa uwekezaji katika maeneo haya unaweza kusaidia kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza tija, kulinda mazingira, na kushughulikia changamoto za muda mrefu kama umasikini na ukosefu wa ajira, hususan kwa vijana na wanawake.
Katika hatua ya utekelezaji, Mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa Benki ya Teknolojia na mashirika mengine ya UN kuongeza kasi kwa kutafsiri mapendekezo ya TNA kuwa miradi halisi.
Amesisitiza kuwa sekta binafsi inapaswa kuwa kiungo muhimu, akitaja maeneo kama Nishati mbadala isiyoegemea kwenye gridi, Majukwaa ya kidijitali kwa kilim, Kiotomatiki katika sekta ya uvuvi.
“Teknolojia hizi si tu kwa utoaji wa huduma bora za umma, bali pia zinaweza kuchochea uwekezaji na kuendeleza ujasiriamali,” ameongeza.
Komatsubara alihitimisha kwa kuahidi kuwa timu ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania iko tayari kusaidia utekelezaji wa mapendekezo ya TNA kupitia mipango ya pamoja, usaidizi wa kiufundi, ujenzi wa uwezo na ushirikiano wa kimkakati.
“Tuko tayari kushirikiana katika kuijenga Tanzania yenye msingi wa kiteknolojia,” amesema.
Akizungumza katika uzinduzi huo, mwakilishi kutoka Benki ya Teknolojia ya Umoja wa Mataifa (UN), Deodat Maharaj amesema uzinduzi wa repoti hiyo ni dira ya mabadiliko kwa Tanzania inayosisitiza kuwa teknolojia haipaswi kuwa chaguo, bali kipaumbele cha maendeleo.
Ameeleza kuwa repoti hiyo imelenga maeneo mablimbali ikiwemo kilimo na uchumi wa buluu, pamoja na sekta mbili zilizopewa kipaumbele katika TNA kwa uwezo wake wa kuleta ajira, kukuza pato la taifa, na kuimarisha maisha ya Watanzania.
Tanzania, ikiwa na fukwe ndefu za zaidi ya kilomita 1,400, imeelezwa kuwa na fursa adimu za kukuza uchumi wa bahari, huku teknolojia zikiainishwa kuwa nyenzo ya kufanikisha ustawi huo.
“TNA hii inalingana kikamilifu na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 na Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya 2024. Inaonesha ni wapi pa kuwekeza, kwa namna gani, na kwanini,” ameongeza.
Katika hitimisho lake, mwakilishi wa Benki ya Teknolojia alisisitiza kuwa TNA si nyaraka ya serikali tu.
“Ni zana kwa sekta binafsi, mashirika ya maendeleo, na hata jumuiya za kimataifa. Inaweka ramani ya uwekezaji, ubunifu na ushirikiano kwa mustakabali wa Tanzania.”
Kwa kuungwa mkono na mashirika kama WEDO na Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu, TNA inatarajiwa kuzalisha miradi ya majaribio yenye tija na kuifanya Tanzania kuwa mfano wa mafanikio ya teknolojia kwa maendeleo kwa nchi zinazoendelea.
Matukio mbalimbali katika picha.