Jimbo la Vunjo limeendelea kuwa miongoni mwa majimbo yenye msisimko mkubwa kila uchaguzi mkuu unapokaribia, lakini awamu hii hali inaonekana kuchukua sura tofauti, baada ya mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Dkt Charles Stephen Kimei, kuonekana kupigiwa upatu na wananchi walio wengi kutetea tena nafasi hiyo.
Kwa mujibu wa maoni yaliyokusanywa na waandishi wetu katika kata mbalimbali za jimbo hilo, wananchi wengi wameeleza kuwa Dkt Kimei ameleta mwelekeo mpya wa uongozi wa uwazi, uwajibikaji na utendaji wa kazi unaoonekana.
Wengi wamemwelezea kama mbunge anayewasikiliza na kuwa karibu na jamii, huku akitajwa kuwa “Mbunge wa vitendo, si maneno.”
Katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake, Dkt Kimei amesimamia miradi kadhaa mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa zahanati na vituo vya afya, uboreshaji wa shule za msingi na sekondari, ujenzi wa barabara za vijijini, pamoja na usambazaji wa umeme kupitia mradi wa REA.
Pia ameendelea kushiriki mijadala ya Bunge kwa nguvu, ambapo ameuliza zaidi ya maswali 100 na kuchangia hoja muhimu zinazogusa maisha ya wananchi wa Vunjo.
Isitoshe, mbunge huyo ameweka rekodi kwa kuwa miongoni mwa viongozi wachache wanaorejea jimboni mara kwa mara kwa ajili ya kusikiliza wananchi, kufuatilia utekelezaji wa miradi, na kushiriki mikutano ya hadhara ya uwajibikaji hali ambayo imewafanya wananchi wengi kuona ni haki kumpa nafasi ya kuendeleza alipoishia.
Hata hivyo, hali ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) si ya kubeza, kwani tayari kuna idadi kubwa ya makada wa chama hicho wanaotajwa kuonesha nia ya kugombea nafasi hiyo kupitia vikao vya ndani vya chama.
Hali hiyo inaashiria ushindani mkali kwenye hatua ya kura ya maoni, ingawa wengi wanabainisha kuwa uteuzi utakaozingatia rekodi ya utendaji unaweza kuimarisha nafasi ya chama hicho kushinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu.
Wananchi kutoka maeneo ya Kirua, Kahe, Njiapanda, Mamba, Makuyuni, Mwika na Marangu wameeleza kuwa japokuwa ushindani ndani ya chama ni ishara ya demokrasia, hawana mashaka na uwezo wa Dkt Kimei kuendelea kuwakilisha vyema Jimbo la Vunjo endapo atapewa tena nafasi hiyo.
“Sisi wananchi wa Vunjo tuna macho, tumeona kazi. Tumesikia mijadala bungeni, tumeona miradi kwenye kata zetu tunachotaka ni maendeleo, si maneno matupu,” alisema Mzee Kessy, mkazi wa Kirua Vunjo Mashariki.
Ikiwa ni takribani siku tano kabla ya mchakato rasmi wa kuchukua na kurejesha fomu za ubunge kuanza ndani ya CCM, macho na masikio sasa yameelekezwa Vunjo jimbo ambalo linabeba historia, ushindani, na matarajio makubwa ya kisiasa.