Banda la NBAA lipo ndani ya jengo la Wizara ya Fedha linawahudumia wananchi kwa kutoa maelekezo ya usajili wa mitihani katika ngazi mbalimbali za taaluma ya uhasibu, pamoja na kutoa maelekezo kuhusu ulipaji wa ada na huduma nyingine muhimu.
Akizungumza na Michuzi Blog, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa NBAA, Magreth Kageya alisema kuwa katika kipindi hiki cha Sabasaba Bodi imewasogezea wananchi huduma karibu kwa kutoa huduma zote kama vile usajili wa watahiniwa wa mitihani ya Bodi, usajili wa wanachama wa ngazi mbalimbali, usajili wa Makampuni, usajili wa kozi mbalimbali zinazoendeshwa na Bodi mfano ‘Certificate na Diploma ya IPSAS’, ‘Professional Diploma in Internal Auditing’ ambayo ni kozi mpya kwa wanaofanya kazi kwenye idara za ukaguzi wa ndani ili kuwasaidia kuwa na uelewa kwenye masuala ya ukaguzi.
Aidha, Bi. Kageya aliongeza kwamba NBAA kwa sasa inatumia mifumo ya kidijitali kutoa huduma zake, ambapo wananchi wanaweza kufikia huduma hizo kupitia tovuti rasmi ya Bodi ambayo ni www.nbaa.go.tz.
Maonesho haya ya Sabasaba ni fursa kubwa kwa Bodi ya NBAA kuwasiliana moja kwa moja na wananchi na wadau mbalimbali wa taaluma ya uhasibu na ukaguzi, ili kuboresha utoaji wa huduma na kuelimisha kuhusu umuhimu wa taaluma hiyo katika maendeleo ya taifa.
Huduma zikiendelea kwenye banda la NBAA